
Waziri Dkt. Rhimo Nyansaho akiwasilisha hotuba yake ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027, Bungeni jijini Dodoma jana.
Dodoma
---------------
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa itaongeza uwekezaji katika zana za kisasa za kijeshi, teknolojia na mafunzo kwa wanajeshi ili kuimarisha ulinzi na usalama wa taifa.
Pia, wizara hiyo imesema itapanua miundombinu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kuwapa vijana wengi mafunzo ya kijeshi na stadi za kazi.
Azma ya wizara hiyo kujiimarisha na kupanua shughuli zake ilielezwa Bungeni jana jijini Dodoma wakati Waziri Dkt. Rhimo Nyansaho alipowasilisha bajeti ya shilingi trilioni 4.2 kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.
Waziri Nyansaho alisema wizara hiyo imepanga kutekeleza majukumu yake kulingana na Dira ya Taifa 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo ya Miaka Mitano, Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 na Ilani ya chama tawala - Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2025-2030.
Alisema sehemu kubwa ya bajeti hiyo itaelekezwa kwenye kuimarisha vifaa vya kisasa vya kijeshi, mifumo ya mawasiliano, mafunzo na rasilimali watu na kuboresha mazingira ya kazi kwa wanajeshi, hasa huduma za afya, makazi, mazoezi na utunzaji wa vifaa vya kijeshi.
Kuhusu JKT, Waziri Nyansaho alisema miundombinu ya jeshi hilo itaboreshwa ili kuwezesha kupokea na kutoa mafunzo kwa vijana wengi, huku hatua zikichukuliwa kuliongezea nguvu Jeshi la Akiba kwa manufaa ya ulinzi wa taifa.
Kwa mujibu wa Waziri Nyansaho, serikali imeweka mkazo kwenye viwanda vipya vya sekta ya ulinzi ambavyo vitazalisha bidhaa za matumizi ya kijeshi na kiraia kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Kama ilivyo kwa siku za nyuma, wizara hiyo itaendeleza ushirikiano wa kimataifa katika ulinzi kupitia Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Ushirikiano huo pia utagusa mamlaka za kiraia katika kukabiliana na majanga, kwa mujibu wa Waziri Nyansaho.

Waziri Nyansaho akisalimiana na viongozi wa juu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kuwasilisha bajeti ya wizara yake Bungeni jana.
Ulinzi mipakani waendelea kuwa shwari
Waziri Nyansaho aliliarifu Bunge kwamba Tanzania ni salama na vyombo vya ulinzi vimekuwa mstari wa mbele na makini mipakani kwa kukabiliana na changamoto zozote ndani na nje ya mipaka hiyo.
Aidha, alisema kumekuwepo na changamoto mbalimbali kama vile uharibifu wa alama za mipaka, uchakavu wa barabara za ulinzi na migogoro ya ndani katika baadhi ya nchi jirani.
Hata hivyo, Waziri Nyansaho alilithibitishia Bunge kuwa mipaka ya Tanzania yenye urefu wa kilomita 5,923.41 inayojumuisha nchi kavu, anga na eneo la maji imeendelea kuwa chini ya ulinzi makini wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia operesheni, doria na ushirikiano wa karibu na vyombo vingine vya usalama.
Mpaka wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasiaa ya Kongo, Waziri alisema nao umeendelea kuwa salama licha ya vurugu za kisiasa katika taifa hilo jirani.
Nao mpaka wa Tanzania na Msumbiji, ulinzi wake unazidi kuimarishwa dhidi ya uwepo wa kikundi cha kigaidi cha Ansar Al- Sunna Wssl Jamaah katika eneo la Cabo Degado, alisema Waziri Nyansaho.
Waziri huyo alisema kwamba kwa kutumia diplomasia, mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi na mpaka kati ya Tanzania na Uganda yote ni shwari.
Kuhusu Bahari ya Hindi, alilieleza Bunge kuwa JWTZ kwa ushirikiano na vyombo vingine vya usalama inaendelea na doria kudhibiti uharamia, wahamiaji haramu, biashara ya dawa za kulevya na ugaidi.
Vilevile, Tanzania kama zilivyo nchi nyingine, inajiimarisha kiteknolojia kwa ajili ya usalama wa anga kuhakikisha unakwenda sambamba na matumizi makubwa ya teknolojia za kisasa duniani.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment