NEWS

Tuesday, 30 June 2026

Gawio Day 2026: Twiga-Barrick yaongoza kwa kutoa shilingi bilioni 221.9 serikalini



Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akipokea gawio la shilingi bilioni 221.9 kutoka kwa Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido (kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya Twiga Minerals, Mathias Chanila, Ikulu jijini Dar es Salaam, leo.

Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
--------------------

Ubia kati ya kampuni ya Barrick na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals umefanya vizuri baada ya kuwa kinara kwa kuipa serikali gawio la shilingi bilioni 221.9 na kutunukiwa tuzo ya nafasi ya kwanza kwa kuongoza kutoa gawio kubwa mwaka huu wa 2026.

Hundi ya mfano ya kiasi hicho cha fefha imekabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, wakati wa hafla ya serikali ya kupokea gawio na michango kutoka taasisi na mashirika ya umma iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam leo.

Rais Samia amezipongeza taasisi na kampuni ambazo serikali ina ubia nazo zinafanya vizuri kwa kutoa gawio na kuongeza tija kwenye biashara na uwekezaji kwa maslahi mapana ya taifa.

Amesema ongezeko la gawio kwa serikali kutoka shilingi trilioni 1.28 hadi trilioni 1.328 na kwamba uzalishaji wenye tija umekuwa ukikua na ufanisi kuongeza kwenye mashirika ya umma, taasisi na kampuni za ndani ya nchi kwa maendeleo ya taifa na watu wake.

“Tunakwenda vizuri na nina jivunia kuwa na viongozi ambao wanaleta matokeo chanya kwa maslahi ya nchi na watu wake. I am very proud of you,” amesema Rais Samia.

Amefafanua kuwa usimamizi wa taasisi za nchini ni muhimu kuwa na viongozi makini na imara kwa maendeleo endelevu ya taifa na watu wake.

Pamoja na mambo mengine, Rais Samia amesisitiza kuwa Gawio Day ni sehemu ya kujipima kuhusu uwekezaji wenye tija ili kuleta maendeleo ya kweli kwa taifa.

Ametoa maelekezo ya kuendelea kuhakikisha kwamba kampuni ambazo serikali ina ubia ni muhimu kuweka mazingira rafiki ili kuwa na mizani ya kunufaisha pande zote kwa maslahi ya taifa na ustawi wa jamii ya Watanzania.

Mwaka jana, Barrick-Twiga ilitoa gawio la shilingi bilioni 93.6, mwaka 2022/23 ilishika nafasi ya kwanza kwa kutoa gawio kwa serikali kiasi cha shilingi bilioni 84, ambapo mwaka wa nyuma yake ilitoa gawio la shilingi bilioni 53.5.

Migodi ya dhahabu iliyopo chini ya Barrick na Twiga Minerals nchini ni North Mara, Bulyanhulu na ule wa Buzwagi uliopo katika mchakato wa kufungwa - ambapo kwa sasa umebadilishwa kuwa kongani maalum la kimataifa la sekta ya madini - ijulikanayo kama Buzwagi Economic Special Zone.

Akzungumzia mafanikio hayo, Dkt. Ngido amesema Barrick na Twiga Minerals mbali na kutoa gawio nono, pia imekuwa ikichangia pato la serikali kupitia malipo ya tozo mbalimbali katika maeneo yenye shughuli za migodi yake sambamba na kuchangia kukuza uchumi wa taifa kupitia ulipaji kodi, ushuru, magawio, mishahara na malipo kwa wazabuni wa ndani tangu ilipoanza ubia na serikali mwaka 2019.

Ameongeza kuwa uwekezaji wa Barrick kupitia utekelezaji wa mkakati wake endelevu, mbali na kuchangia pato la taifa kwa ajili ya ukuzaji uchumi wa nchi, pia unaendelea kuboresha maisha ya jamii zilizo jirani na migodi yake kupitia ufanikishaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), hususan katita sekta za elimu, afya, maji safi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara.

Uwekezaji wa kampuni ya Barrick nchini pia unaendelea kukuza biashara za ndani kwa kunufaisha wazabuni na wakandarasi wazawa inaofanya nao kazi na kuongeza wigo wa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja nchini.

Mafanikio yanayozidi kupatikana kutokana na ubia wa Barrick na Twiga nchini ni kielelezo cha uchimbaji madini endelevu unaoweka uwiano baina ya uwajibikaji wa kiuchumi, kimazingira na kijamii.

Kwa upande wake Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema kwamba Siku ya Gawio ni muhimu kuendelea kujithamini katika juhudi za mageuzi ya kiuchumi na kimkakati ili kuendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa 2020-2050.

Awali, akizungumza kwenye hafla hiyo ambayo ilikuwa na kaulimbiu “Uwekezaji wenye matokeo ya nguvu ya ushindani wa Dira 2020-2050”, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema tukio hilo ni muhimu na kwamba Rais Samia amelipa uzito kutokana na umuhimu wa michango na gawio la hisa kwa uchumi na uwekezaji wa taifa.

Mchechu ameongeza kuwa mashirika ya umma na kampuni zilizopo nchini zina mchango mkubwa kwenye kukuza na kuboresha huduma za kijamii kwa Watanzania pamoja na kuchangia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

“Mheshimiwa Rais, kwa maelekezo na maono yako juu ya mageuzi ya kiuchumi na ya kiutawala na mikakati ya mipango ya utekelezaji wa miradi na kazi imeleta ufanisi kwenye biashara na kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na kukuza ajira hapa nchini,” ameongeza Mchechu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages