![]() |
| Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba |
Na Mwandishi Wetu,
Mara
------------------------------------------
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi katika mkoa wa Mara kuanzia kesho Jumatano, kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Ratiba iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa, Kanali Evans Mtambi, inaonesha kwamba ziara hiyo itafanyika Julai 1 hadi 5, 2026, ambapo Waziri Mkuu Mwigulu atatembelea wilaya, halmashauri na majimbo yote 10 ya uchaguzi ya mkoa huo.
Katika taarifa yake kwa umma, Kanali Mtambi aliongeza kuwa Waziri Mkuu pia atetembelea na kukagua miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 52.9.
Ratiba hiyo, inaonesha kuwa Julai 1 mchana, Waziri Mkuu Mwigulu atawasili katika wilaya ya Serengeti asubuhi, ambapo atakagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuhutubia mkutano wa hadhara.
Baadaye siku hiyo hiyo mchana ataelekea Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, ambapo atahutubia, kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika Uwanja wa Shule ya Sekondari Ingwe, Nyamongo.
Kesho kutwa Julai 2, Waziri Mkuu Mwigulu atakuwa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime, ambapo atatembelea, kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara, kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Uwanja wa Serengeti - maarufu Shamba la Bibi.
Hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote yaliyopangwa kufanyika mikutano hiyo ili kumpokea Waziri Mkuu, kusikiliza maelekezo yake na kutumia fursa hiyo kuwasilisha kero, changamoto na maoni yao.
Kwa mujibu wa Meja Gowele, ziara hiyo ni fursa muhimu kwa wananchi wa Tarime kueleza moja kwa moja changamoto zinazowakabili mbele ya Kiongozi Mkuu wa Shughuli za Serikali.
”Kwa hiyo, wananchi wote tujitokeze kwa wingi kwa ajili ya kumpokea Waziri Mkuu, lakini pia twende tukatoe kero na changamoto ambazo tunazo. Sisi tunashukuru sana kwa ujio wake ambapo tunaamini anakuja kuleta faraja kwa wananchi.
“Tujitokeze kwa wingi kumsikiliza Waziri Mkuu ili aweze kutoa utatuzi wa changamoto ambazo yawezekana kwa namna moja ama nyingine hazikuweza kushughulikiwa au zinahitaji uamuzi wake,” alisisitiza Meja Gowele.

No comments:
Post a Comment