
Na Godfrey Marwa
Tarime
------------

Tarime
------------
Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) CCM Mkoa wa Mara, Sophia Lucas Maregesi, ameitaka UWT Wilaya ya Tarime kubuni na kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayoiwezesha jumuiya hiyo kujitegemea kuanzia ngazi ya matawi.
Akihutubia mkutano wa UWT CCM Wilaya ya Tarime jana, Sophia alisema uhai na uimara wa chama hicho tawala na jumuiya zake unategemea uwezo wa kujitegemea kiuchumi, hivyo akasisitiza umuhimu wa kuwa vyanzo vya mapato vitakavyosaidia kujiendesha.
"Twendeni tukaibue miradi ya jumuiya na kuanzisha vitega uchumi, uhai wa chama ni kujitegemea kiuchumi, tuepuke kuwa tegemezi kuanzia ngazi ya tawi, kata na wilaya,” alisema.

Katibu Sophia akizungumza katika mkutano huo.
Aidha, Sophia aliwataka viongozi wa UWT kuendelea kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuhakikisha vikao vya chama vinafanyika kwa wakati, wanachama wapya wanaandikishwa na ada za uanachama zinalipwa kwa wakati.
"Kufanya vikao vya chama, kuingiza wanachama wapya, ulipaji ada, ndio uhai wa chama,” alisisitiza Sophia.
Sophia pia aliwahimiza viongozi na wanachama wa UWT kuendelea kuhubiri amani, upendo na mshikamano, akieleza kuwa hayo ni maadili yaliyoasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, pamoja na kuendelea kueleza utekelezaji wa kazi zinazofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Tarime, Neema Charles, alimshukuru Katibu huyo wa UWT Mkoa kwa ziara yake, akisema imekuwa chachu ya kuimarisha umoja, mshikamano na utendaji kazi wa viongozi wa jumuiya hiyo.
Neema alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa viongozi wa UWT kuanzia ngazi ya matawi hadi wilaya kutekeleza majukumu yao kwa bidii, ushirikiano na kuheshimiana ili kuendelea kuijenga na kuiimarisha jumuiya hiyo.
"Twende tukafanye kazi kwenye matawi yetu, tujue majukumu yetu, tuheshimiane kwa nafsi tulizonazo, tukijua majukumu hakuna kitakachotusumbua,” alisema Neema.
(Picha zote na Mara Online News)

No comments:
Post a Comment