
Na Christopher Gamaina
Tarime
---------------


Mbunge Esther Matiko kikaoni
Tarime
---------------
Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, Esther Matiko, amewakutanisha wadau wa maendeleo katika kikao maalum cha kujadili mwelekeo wa maendeleo ya kisekta katika jimbo hilo la mkoani Mara.
Kikao hicho ambacho kilishirikisha makundi tofauti ya jamii na taasisi mbalimbali, kilifanyika jana katika Hoteli ya CMG mjini Tarime, mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Gowele.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho, Meja Gowele alimpongeza Mbunge Matiko kwa ubunifu wa kuandaa kikao hicho, akisema ni hatua muhimu inayowapa wananchi nafasi ya kushiriki moja kwa moja kujadili maendeleo yao.
Alisema ushirikiano wa viongozi na wananchi ndiyo msingi wa maendeleo endelevu, hivyo akawahimiza wakazi wa Tarime Mjini kuendelea kumpa ushirikiano mbunge huyo ili aweze kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi.
Aliwahamasisha wananchi kutumia kikamilifu fursa zilizopo katika sekta za kilimo, ufugaji na madini pamoja na kuendelea kuitunza amani iliyopo, akisisitiza kuwa ndiyo nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, Meja Gowele aliwataka wataalamu wa Halmashauri ya Mji wa Tarime kuongeza juhudi katika kuwawezesha vijana kwa kuwasaidia kusajili vikundi vyao ili viweze kunufaika na mikopo ya halmashauri pamoja na kazi mbalimbali waweze kujiongezea kipato na kujikomboa kiuchumi.

Mkuu wa Wilaya alitumia nafasi hiyo hiyo pia kutoa wito kwa wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu wa wilaya hiyo kwa kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuchochea migogoro au kuvuruga mshikamano wa jamii.
Awali, akizungumza katika kikao hicho, Mbunge Matiko alisema atafanya kikao hicho kuwa cha kila mwaka baada ya kumalizika kwa Bunge la Bajeti, ili kutoa mrejesho wa shughuli za kibunge na kupokea maoni ya wananchi kuhusu masuala yanayowahusu.
Alisema utaratibu huo utaongeza uwajibikaji na kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi na wananchi katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazolikabili jimbo hilo.
Mbunge huyo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha zinazowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Mji wa Tarime, ikiwemo kuboresha huduma za kijamii na kukuza shughuli za kiuchumi.
Aidha, aliwahimiza wananchi kuendelea kuilinda amani ya nchi, akieleza kuwa ni moja ya tunu muhimu za taifa zinazowezesha maendeleo na ustawi wa Watanzania.
Mbunge Matiko alisisitiza kuwa ataendelea kusikiliza maoni, mapendekezo na changamoto za wananchi wa Tarime Mjini ili kuziwasilisha bungeni na kuzifuatilia kwa mamlaka husika hadi zipatiwe ufumbuzi.

Mbunge Esther Matiko kikaoni
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Thobias Elias Ghati, alimpongeza Mbunge Matiko kwa juhudi zake za kuwawakilisha vizuri wananchi wa Tarime Mjini katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwenyekiti Thobias alisema mbunge huyo amekuwa akiwasilisha kwa ufanisi changamoto za wapigakura wake na kuiombea halmashauri hiyo miradi mbalimbali ya maendeleo ya kisekta.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa wadau mbalimbali kutoa maoni na mapendekezo kuhusu namna ya kuharakisha maendeleo ya Tarime Mjini, huku msisitizo mkubwa ukiwekwa katika ushirikiano, matumizi bora ya fursa za kiuchumi na ulinzi wa amani ili kuchochea maendeleo endelevu ya jimbo hilo.
No comments:
Post a Comment