
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Juni 229, 2026.
Musoma
---------------
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kwa mshikamano, utulivu na uchapakazi ulioiwezesha kukusanya mapato ya ndani kiasi cha shilingi bilioni 2.9 sawa na asilimia 104, ambapo lengo lilikuwa kukusanya shilingi bilioni 2.8.
Pia, Kanali Mtambi ameipongeza halmashauri hiyo kwa kupata hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Kiongozi huyo wa mkoa alitoa pongezi hizo Juni 29, 2026, katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, kilichojadili hoja za CAG katika mwaka huo wa fedha.

"Niwapongeze kuepusha migogoro isiyo na tija, baraza lililopita kulikuwa shughuli.. baraza lenu limetulia, muendelee hivyo kujadili mambo yatakayoleta maendeleo kwa wananchi.
"Hongereni sana, nikutakeni mhakikishe asilimia za mapato zinaenda juu hadi bilioni tatu mwaka ujao, pia hongereni kwa hati safi kutoka kwa CAG,” alisema Kanali Mtambi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Wakili Msongela Palela, alimshukuru Mkuu wa Mkoa na kumuahidi kufanyia kazi ushauri na maelekezo yake.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Samwel Okelo, alimshukuru Kanali Mtambi akisema: "Nikushukuru, tutakuwa makini, kwa pamoja tutahakikisha tunaenda vizuri.”
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment