
Mkurugenzi wa MUWASA, Esther Gilyoma, akitoa taarifa ya urejeaji wa huduma ya maji katika maeneo yaliyokuwa yamekumbwa na changamoto mjini Musoma jana.
Musoma
----------------
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), mkoani Mara imethibitisha kurejea kwa huduma ya maji katika maeneo ya Kwangwa, Nyabange, Buhare na Nyabisare baada ya kutatua changamoto ya kiufundi iliyosababisha wananchi kukosa huduma hiyo kwa takribani wiki mbili hadi tatu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa MUWASA, Esther Gilyoma, hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo hayo imerejea katika kiwango cha kawaida kufuatia ushirikiano kati ya MUWASA na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika kutatua tatizo la umeme mdogo (low voltage) lililoathiri uendeshaji wa mitambo ya kusukuma maji.
“Maeneo haya yalikumbwa na kadhia ya ukosefu wa maji kwa wiki kama mbili tatu hivi kutokana na changamoto ya usukumaji katika mitambo yetu. Tulihitaji umeme wa kutosha kwa ajili ya kusukuma pampu saba kwa wakati mmoja, jambo ambalo halikuwezekana kutokana na low voltage,” alisema
Alieleza kuwa baada ya kubaini chanzo cha tatizo hilo, MUWASA ilifanya kazi kwa karibu na TANESCO, ambao walifika katika mitambo husika na kufanikisha utatuzi wa changamoto ya umeme iliyokuwa ikikwamisha usambazaji wa maji.
“Tumejiridhisha kwamba maji yanatoka na wateja wanaendelea kushukuru sana serikali yao kupitia MUWASA, ambapo sisi tumetimiza wajibu wetu kuwapatia maji, lakini nao wanafurahi kwamba huduma ya maji imerejea, na hii sasa ni furaha kwetu sote kwamba mteja anahitaji maji na wala hahitaji maneno,” alisema Gilyoma.
Mkurugenzi huyo alisema katika ziara hiyo pia alitembelea tenki la Nyabange, eneo ambalo limekuwa likilalamikiwa mara kwa mara kutokana na changamoto ya upatikanaji wa maji iliyojitokeza hivi karibuni.
Alikiri kuwa wananchi wa Nyabange walipitia kipindi kigumu kutokana na ukosefu wa huduma hiyo muhimu na kuwaomba radhi kwa usumbufu uliotokea.
“Niwaombe radhi wateja wa Nyabange kwa hali iliyojitokeza, lakini pia niwaombe sasa waendelee kutumia maji hayo kwa uadilifu ili kuendelea kufurahia huduma, walinde pia miundombinu na kulipa bili zao kwa wakati ili MUWASA iendelee kutoa huduma endelevu,” alisema.
Mkurugenzi Gilyoma aliipongeza Serikali, Wizara ya Maji na TANESCO kwa ushirikiano na maelekezo yaliyowezesha kutatuliwa kwa changamoto hiyo kwa haraka.
Alisema MUWASA imejipanga kuhakikisha huduma ya maji inaendelea kuwa endelevu kwa wananchi na kuwaomba wateja kuendelea kushirikiana na mamlaka hiyo kwa kulinda miundombinu ya maji pamoja na kulipa bili kwa wakati.
“Mipango yetu ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma endelevu itolewayo na MUWASA. Huduma hii ya maji ni endelevu na sio suala la jana na leo tu, sisi tumejipanga kwa ajili ya kuwahudumia, tunaomba ushirikiano wao - walinde miundombinu ya maji, walipe bili kwa wakati ili MUWASA iendelee kutoa huduma endelevu,” alisema Gilyoma.
Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa MUWASA imefanikiwa kuvuka lengo la Ilani ya CCM la kufikia asilimia 95 ya wananchi wanaopata majisafi mijini kufikia 2025, ambapo imefikia asilimia 98 ya wanaopata huduma hiyo katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.
Mbali na Manispaa ya Musoma, mamlaka hiyo pia inasambaza huduma ya majisafi kwa wakazi wa miji ya Shirati wilayani Rorya, Mugumu wilayani Serengeti na Tarime.



No comments:
Post a Comment