
Mkurugenzi wa Shirika la Sheria na Haki za Binadamu la Tuwakombowe Paralegal, Bonny Matto.
Tarime
--------------
Shirika la Sheria na Haki za Binadamu la Tuwakombowe Paralegal limeipongeza Kampuni ya Barrick kwa kuanzisha kliniki ya kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, likisema ni mfano bora unaopaswa kuigwa na migodi mingine ili kuimarisha mahusiano na jamii inayoizunguka.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa shirika hilo ambalo linatekeleza shughuli zake katika wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara, Bonny Matto, kliniki hiyo inawawezesha wananchi kuwasilisha malalamiko yao kwa urahisi na kupata ufumbuzi, hali itakayosaidia kuboresha maelewano baina ya pande hizo mbili.
“Uanzishwaji wa kliniki hii ni hatua muhimu sana kwani itawezesha wananchi kusikilizwa na kupata ufumbuzi wa changamoto zao kwa wakati. Inaweza isimalize kabisa lakini ninaamini itasaidia kupunguza migogoro na kuimarisha uelewano kati ya wananchi na mgodi,” amesema Matto katika mazungumzo na Mara Online News, mjini Tarime, leo Jumapili, Juni 21, 2026.
Aidha, aliwataka wananchi kutofautisha malalamiko yanayohusu shughuli za mgodi na yale yanayohusu majukumu ya serikali ili kuepusha mkanganyiko unaoweza kuathiri ufanisi wa utatuzi wa changamoto hizo.
Matto alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakielekeza kwa mgodi hata malalamiko ambayo kimsingi yanapaswa kushughulikiwa na taasisi za serikali, jambo ambalo linaweza kuchelewesha upatikanaji wa suluhisho sahihi.
“Ni muhimu wananchi wakatambua mipaka ya majukumu. Siyo kila changamoto inayotokea katika jamii inahusiana na mgodi. Kuna masuala ambayo yanapaswa kushughulikiwa na serikali kupitia mamlaka zake husika, na mengine yanayohusu moja kwa moja mgodi. Kutambua tofauti hiyo kutasaidia kila upande kuwajibika ipasavyo,” alisisitiza.
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.
Hivi karibuni, mgodi huo ulizindua kliniki ya kusikiliza na kushughulikia malalamiko na maoni ya wananchi katika vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo, ikiwa ni mwendelezo wa kuimarisha zaidi mahusiano na jamii inayouzunguka.
Vijiji hivyo ni Mjini Kati, Nyangoto, Kewanja, Matongo, Nyabichune, Kerende, Nyakunguru, Komarera, Genkuru, Msege na Nyamwaga.
Ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ushiriki mpana wa wadau wote, klinki hiyo ina kamati inayojumuisha wafanyakazi wa mgodi huo, madawati ya malalamiko kutoka ofisi za Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, asasi za kiraia na wawakilishi wa jamii.
No comments:
Post a Comment