NEWS

Monday, 29 June 2026

Uvamizi wavuvi Ziwa Victoria umedhibitiwa – RC



Kanali Mtambi (katikati) akizungumza na Kanali Manaki ofisini kwake mjini Musoma wiki iliyopita.

Na Mwandishi Wetu
Musoma
---------------

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amesema vitendo vya kuvamia wavuvi katika Ziwa Victoria mkoani humo sasa vimedhibitiwa kwa kiasi kikubwa kufuatia kuimarishwa kwa ulinzi na doria za pamoja.

Kanali Mtambi alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Musoma wakati alipompokea na kufanya mazungumzo na Kanali Ally Manaki kutoka Makao Makuu ya Kamandi ya Jeshi la Wanamaji nchini.

Alisema mafanikio ya kudhibiti uvamizi kwa wavuvi yametokana na ushirikiano madhubuti kati ya Serikali ya Mkoa wa Mara na Jeshi la Wanamaji, ambao umewezesha kuimarishwa kwa operesheni za kiusalama ndani ya Ziwa Victoria na maeneo ya mipakani.

Kiongozi huyo wa mkoa alitumia nafasi hiyo kuishukuru Kamandi ya Jeshi la Wanamaji kwa ushirikiano wake kwa Serikali ya Mkoa wa Mara katika kupambana na wavamizi wa wavuvi Ziwa Victoria.

Vilevile, aliipongeza Kamandi hiyo kwa ushirikiano inaoupatia mkoa huo katika doria endelevu za kulinda usalama wa mipaka ya nchi, rasilimali na wavuvi wa Tanzania katika ziwa hilo la kimataifa.

Kwa muda mrefu, wavuvi katika Ziwa Victoria upande wa Tanzania, hususan katika wilaya za Rorya na Musoma mkoani Mara, wamekuwa wakilalamika kuvamiwa na wahalifu wanaodaiwa kutoka nchi jirani, ambao huwapora samaki, zana za uvuvi na kuhatarisha maisha yao.

Hivyo, kuimarishwa kwa ulinzi na doria kutarejesha hali ya usalama kwa wavuvi na kuchochea ukuaji wa shughuli za uvuvi katika eneo hilo.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages