NEWS

Monday, 29 June 2026

Kamati ya Siasa CCM Mara yakagua utekelezaji miradi ya maendeleo



Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi (wa pili kulia mbele), akiwa katika ukaguzi wa ujenzi wa vibanda 135 vya biashara katika Halmashauri ya Mji wa Tarime. Aliyevaa koti jekundu ni Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Gimbana Ntavyo.

Na Mwandishi Wetu
Mara
-------------

Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara imeonesha kuridhishwa na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo, huku ikisisitiza umuhimu wa usimamizi mzuri ili iweze kutoa huduma bora na kuongeza tija kwa wananchi.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi, aliongoza kamati hiyo hivi karibuni katika ziara ya kukagua miradi ya elimu, afya, biashara na miundombinu ya barabara inayotekelezwa kwa fedha za Serikali Kuu na mapato ya ndani ya halmashauri, yakiwemo ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

Akiwa wilayani Tarime, Chandi alikagua jengo jipya la utawala katika Shule ya Sekondari Mjini Kati iliyopo Nyamongo, lililojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 172 kupitia fedha za CSR kutoka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaoendeshwa na Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Twiga Minerals.

Alisema uwekezaji huo unaonesha mchango wa sekta binafsi katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha huduma za elimu, huku akiwataka watumishi wa shule hiyo kutumia jengo hilo jipya kuongeza ufanisi wa kazi.

Aidha, Chandi aliiagiza TANESCO Wilaya ya Tarime kuhakikisha huduma ya umeme inaunganishwa haraka katika jengo hilo ili shughuli za kiutawala zianze bila kuchelewa na kuongeza ubora wa utoaji wa huduma.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, aliwapongeza viongozi wa kijiji, madiwani, mkandarasi, wataalamu kutoka Barrick North Mara na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa usimamizi na ushirikiano uliofanikisha kukamilika kwa mradi huo.

Katika ziara hiyo, Kamati ya Siasa pia ilikagua daraja jipya katika Mto Tighite linalounganisha kata za Matongo na Kibasuka, mradi unaotarajiwa kuboresha mawasiliano na usafiri kwa wananchi wa maeneo yanayozunguka Mgodi wa North Mara.

Vilevile, kamati hiyo ilitembelea mradi wa ujenzi wa vibanda 135 vitakavyokodishwa kwa wafanyabiashara katika Halmashauri ya Mji wa Tarime, mradi ambao unatekelezwa kwa shilingi milioni 395 kutokana na mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.

Kamati ilielezwa kuwa katika mwaka huu wa fedha zimetengwa shilingi milioni 250 kwa ajili ya mradi huo, ambapo shilingi milioni 128 tayari zimetumika katika maandalizi ya eneo, malipo ya mafundi, ununuzi wa mali ghafi na vifaa vya ujenzi.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Chandi aliipongeza Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kutumia mapato yake ya ndani kuanzisha mradi wenye manufaa kwa halmashauri hiyo, wafanyabiashara na uchumi wa eneo hilo.

“Halmashauri ikiwa na vyanzo vyake vya mapato ya ndani vinaisaidia kuendesha shughuli zake bila utegemezi,” alisema Chandi.

Ikiwa wilayani Rorya, Kamati hiyo ya siasa ilikagua ujenzi wa Kituo cha Afya Kuruya, ambacho kimefikia asilimia 92 ya utekelezaji baada ya kutumia shilingi milioni 365.5.

Chandi aliishukuru serikali akisema kituo hicho kitapanua upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.

Mwenyekiti huyo aliwaagiza wahusika kuongeza kazi ya ujenzi ili kufikia mwanzoni mwa Julai 2026 mradi huo ukamilike, lakini pia kuhakikisha huduma ya umeme inaunganishwa kituo hicho kianze kutoa huduma kwa ufanisi.

Kamati hiyo pia ilikagua ujenzi wa Kituo cha Afya Kyang'ombe wilayani Rorya, ambacho kimetengewa shilingi milioni 250.

Mradi huo umefikia asilimia 90 ya utekelezaji na tayari shilingi milioni 160 zimeshtumika.

Katika hatua nyingine, Kamati ya Siasa ilikagua daraja la mawe katika Mto Nyathorogo wilayani Rorya, lililojengwa na kukamilika mwaka huu kwa gharama ya shilingi milioni 729 kutoka Serikali Kuu kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

Daraja hilo linatarajiwa kurahisisha usafiri, kuimarisha mawasiliano na kuwezesha usafirishaji wa bidhaa katika kata ya Nyathorogo na maeneo ya jirani.

Chandi alisisitiza umuhimu wa viongozi kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa tija na wananchi wanapata huduma zilizokusudiwa kwa wakati.

Mwenyekiti Chandi alitumia nafasi hiyo pia kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha zinazowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wa Mara.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages