NEWS

Friday, 19 June 2026

Mara: Wachimbaji wadogo wajengewa uelewa sheria za uchimbaji madini



Mchimbaji mdogo wa madini, Jackson Ngasa Ndakama, akizungumza jana mjini Musoma katika mafunzo maalum kwa wachimbaji wadogo wa madini wa mkoani Mara yaliyoandaliwa na Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini nchini.

Na Godfrey Marwa,
Musoma
--------------

Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini nchini imezindua semina ya mafunzo maalum kwa wachimbaji wadogo zaidi ya 200, pamoja na wadau wa madini mkoani Mara kuhusu sheria za madini, ardhi, usalama wa afya, mazingira na msaada wa kiufundi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo mjini Musoma jana, Mwanasheria Mwandamizi kutoka Wizara ya Madini, Raymond Baravuga, alisema yanalenga kupunguza migogoro kati ya wenye leseni za uchimbaji madini na wamiliki wa ardhi.

"Kawaida ili mchimbaji aweze kuchimba bila kuvunja sheria lazima awe na leseni ya uchimbaji na inakuwa na masharti, ikiwemo kujitambulisha kwa mwenye ardhi kupitia kwa mamlaka za serikali za mitaa.

"Sheria iliyopo - kanuni za msaada wa kiufundi zilizotoka Aprili 2025 zimewatambua wenye maduara. Mwenye leseni anapopata mwezeshaji anao wajibu wa kumfidia mwenye duara kabla ya ule mkataba wa msaada wa kiufundi kuanza kutekelezwa,” alisema Baravuga.

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Madini, Dkt. Anold Ainory, akisema mafunzo hayo yatawajengea wachimbaji hao uelewa utakaowawezesha kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuepuka migogoro.

Dkt. Ainory akizungumza katika mafunzo hayo.

Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, David Mapunda, alisema mafunzo hayo yataendelea kufikisha elimu kwenye maeneo mbalimbali ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini ili kupunguza migogoro inayojitokeza mara kwa Mara.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Mara, David Bitta, aliishukuru serikali kwa kuleta mafunzo hayo akisema yatawasaidia kuepuka migogoro katika utekelezaji wa shughuli zao.

"Yaliyozungumzwa yamekuwa tija na wachimbaji wameitika, kuna vitu vingi walikuwa hawajui, wametambua namna ya kila mmoja kusimamia nafasi yake kati ya mwenye leseni [ya uchimbaji madini] na mwenye ardhi,” alisema Bitta.

Bitta alitumia fursa hiyo pia kuiomba serikali kupitia Wizara ya Madini kupunguza tozo ambazo ni kero kwa wachimbaji wadodo wa madini nchini.

Naye mmoja wa wachimbaji hao, Jackson Ngasa Ndakama, aliishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kuwakumbusha taratibu za kisheria katika mnyororo wa thamani wa uchimbaji madini.

“Tumefundishwa haki ya mmiliki wa leseni na haki ya mmiliki wa ardhi, migogoro ambayo imekuwa ikiendelea maeneo ya kazi itapungua. Taratibu zikifuatwa itasaidia kupunguza migogoro katika sehemu za kazi, lakini pia tumefundishwa kuwa na uchimbaji salama,” alisema Ndakama.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages