NEWS

Sunday, 28 June 2026

Waziri Nyansaho ahitimisha Mafunzo ya Ukamanda, Unadhimu Chuo cha Duluti



Waziri wa Ulinzi na JKT, Dkt. Rhimo Nyansaho, akizungumza jana katika mahafali ya wahitimu mafunzo ya Ukamanda na Unadhimu kwenye Chuo cha Duluti, mkoani Arusha.

Na Mwandishi Wetu
Arusha
--------------

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dkt. Rhimo Nyansaho, juzi alihitimisha rasmi mafunzo ya mwaka mmoja ya Kozi ya Ukamanda na Unadhimu katika Mahafali ya 40 ya Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Tanzania, yaliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Duluti, mkoani Arusha.

Mahafali hayo ambayo Waziri Nyansaho alikuwa mgeni rasmi, yalihusisha maafisa wahitimu 82 kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na nchi rafiki mbalimbali.

Mbali na kuhitimu Kozi ya Ukamanda na Unadhimu, wahitimu hao pia walitunukiwa Shahada za Umahiri na Stashahada katika masuala ya Ulinzi na Usalama, mafunzo yaliyotolewa sambamba na kozi hiyo ili kuwawezesha kupata maarifa ya kina kuhusu ulinzi, usalama na uongozi wa kimkakati.

Akizungumza katika mahafali hayo, Waziri Nyansaho aliwapongeza wahitimu kwa mafanikio yao, akisema kuhitimu kozi hiyo ni ushahidi wa bidii, nidhamu, ujasiri, uthabiti na kujitolea kwao katika kipindi chote cha mafunzo.

Picha ya pamoja

Waziri Nyansaho alibainisha kuwa kozi hiyo ni miongoni mwa mafunzo ya kijeshi yanayotambulika kimataifa na kwamba wahitimu wanapaswa kujivunia mafanikio hayo makubwa.

"Mmethibitisha uwezo wa kukabiliana na changamoto za mafunzo makali na mmeonesha sifa za uongozi zinazohitajika kwa viongozi wa kijeshi sasa na baadaye.

“Mafanikio haya ni hatua muhimu katika safari yenu ya uongozi na utumishi kwa mataifa yenu," alisema Dkt. Nyansaho.

Aidha, waziri huyo aliushukuru uongozi wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu chini ya Mkuu wa chuo hicho, Meja Jenerali Stephen Mnkande, kwa maandalizi mazuri ya mafunzo hayo na kwa kumpa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo.

Alisisitiza kuwa majeshi ya ulinzi yanaendelea kuwa alama ya umoja wa kitaifa, uhuru na mshikamano wa mataifa.

Mbali na jukumu la msingi la kulinda mipaka na mamlaka ya nchi, alisema majeshi ya ulinzi yameendelea kuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na maafa, kujenga miundombinu, kushiriki katika shughuli za maendeleo ya taifa na operesheni maalum.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages