
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akikabidhi Cheti cha Shukrani kwa Mwenyekiti wa REU, Jacob Karoli, leo Jumapili. Anayepiga makofi ni Katibu Mtendaji wa umoja huo, Christopher Gamaina.
Tarime
--------------
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, ameutunuku Umoja wa Kuwezesha Waandishi wa Habari (REU) katika wilaya hiyo Cheti cha Shukrani kama ishara ya kutambua na kuthamini mchango wa wanachama wa umoja huo katika kuitangaza wilaya hiyo vizuri kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Meja Gowele amekabidhi cheti hicho leo Jumapili, Juni 26, 2026, kwa Mwenyekiti wa REU Wilaya ya Tarime, Jacob Karoli na Katibu Mtendaji, Christopher Gamaina, katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ofisi za umoja huo zilizopo mjini Tarime.
Amesema Ofisi ya Mkuu wa Wilaya imeona umuhimu wa kuitunuku REU Cheti cha Shukrani ili kuonesha kutambua na kuthamini ushirikiano wa waandishi wa habari, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kiongozi huyo wa wilaya ameongeza kuwa wanachama wa REU wamekuwa mstari wa mbele katika kuandika na kuripoti habari zinazohamasisha amani, kuimarisha usalama na kutangaza utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayonufaisha wananchi.

“Niwashukuru waandishi wa habari, mmekuwa mstari wa mbele katika kuihabarisha jamii kuhusu mambo mazuri yanayofanyika Tarime - mmeipara wilaya yetu rangi nzuri, lazima kama serikali tutambue na kuthamini mchango wenu mkubwa,” amesema Meja Gowele.
Kwa upande wao, viongozi wa REU Wilaya ya Tarime wamemshukuru kiongozi huyo wa serikali wilayani Tarime kwa kutambua mchango wa waandishi wa habari, wakisema hatua hiyo ni ishara ya kuthamini nafasi ya vyombo vya habari katika maendeleo ya jamii.
Aidha, wamemuahidi Meja Gowele kuwa REU itaendelea kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na viongozi wengine wa serikali wilayani Tarime katika kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi, zenye kujenga na kuhamasisha maendeleo ya kisekta.
Wametaza habari hizo kuwa ni pamoja na zinazotangaza fursa za uwekezaji, maendeleo ya kisekta na mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya kijamii na kimkakati ili kuongeza uelewa wa wananchi, kuvutia na kushawishi wadau mbalimbali kushiriki katika kukuza uchumi wa wilaya ya Tarime.

(Picha zote na REU Wilaya ya Tarime)
Wachambuzi wa masuala ya uongozi na habari wameitaja hatua hiyo ya Mkuu wa Wilaya kuitunuku REU Cheti cha Shukrani kama ishara ya kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na vyombo vya habari kwa maendeleo ya wananchi ya kijamii na kiuchumi.
No comments:
Post a Comment