
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, tuzo ya mlipa kodi kinara.
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick yenye ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals imeendelea kushikilia rekodi ya kulipa kodi kubwa kwa serikali baada ya kutangazwa na kutunukiwa Tuzo ya Rais ya Mlipa kodi Mkubwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025.
Tuzo hiyo ilitangazwa na kutolewa wakati wa hafla ya siku ya kutoa tuzo kwa walipa kodi wakubwa iliyoambatana na maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika hafla hiyo, Rais Samia amepongeza kampuni na taasisi ambazo zimekuwa zikilipa kodi kwa uaminifu na kuwezesha serikali kupata fedha za kuimarisha uchumi wa nchi na kufanikisha kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ustawi wa wananchi.
Tuzo hiyo kwa Barrick ni mwendelezo wa kutambuliwa mchango wake katika kuchangia pato la taifa kwa njia ya kodi, ambapo katika miaka iliyopita pia ilishinda hii na kutambuliwa na TRA miongoni mwa kampuni zinazoongoza kulipa kodi kubwa nchini.
Mbali na kupata tuzo hiyo ya kodi, Barrick-Twiga mwaka huu pia imekuwa kinara wa kutoa gawio kwa serikali, ambapo imetoa kiasi cha shilingi bilioni 221.9.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika picha ya pamoja na Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido na baadhi ya viongozi wa kampuni nyingine zinazolipa kodi kubwa serikalini.
Migodi ya dhahabu inayoendeshwa chini ya ubia wa Barrick na Twiga Minerals nchini ni North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi ambao upo katika mchakato wa kufungwa na kwa sasa umegeuzwa kuwa Kongani Maalum ya Kimataifa ya Sekta ya Madini inayojulikana kama Buzwagi Economic Special Zone.
Barrick pia imekuwa ikichangia pato la serikali kupitia malipo, magawio, mrabaha, tozo mbalimbali na mdau mkubwa wa kuchagia uchumi wa kijamii kupitia mtandao wa biashara zake.
Akizungumzia mafanikio hao kwa kampuni kuendelea kufanya mambo makubwa ya kuleta maendeleo nchini, Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, amesema utekelezaji wa mikakati endelevu ya kampuni kwa ubia na serikali unaendelea kuleta matokeo bora na kuwezesha wananchi kunufaika na rasilimali za madini.
Barrick pia imekuwa ikitekeleza sera ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa ufanisi, ambapo kwa kiasi kikubwa imefanikisha kutekeleza miradi ya kijamii katika maeneo yanayozunguka migodi yake, hususa ni katika sekta za elimu, afya, maji safi na salama pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara.
No comments:
Post a Comment