
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akisalimiana na viongozi mbalimbali mara baada ya kuwasili mkoani Mara jana kwa ziara ya kikazi.
Tarime
---------------
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Bunge lijalo la Agosti 2026 lifute sheria ya kutaifisha mifugo ya wananchi inayokamatwa ndani ya hifadhi za wanyamapori nchini.
Amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kubaini kuwa sheria hiyo ina madhara makubwa kwa wananchi, ikiwemo kuwafilisi wananchi, kuwasababishia umaskini na kudhoofisha ustawi wa familia nyingi zinazotegemea mifugo kuendesha maisha yao.
“Tunakwenda kuifuta hiyo sharia,” alisisitiza Dkt. Mwigulu wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika uwanja wa Shule ya Sekondari Ingwe iliyopo Nyamongo, wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba
Wakati huo huo, Waziri Mkuu huyo alisema mkutano wa Bunge uliopita ulipitisha sheria inayotaka miradi ya ujenzi wa barabara iliyokuwa ikisuasua katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo wilaya ya Tarime na mkoa wa Mara sasa ikamilishwe bila kucheleweshewa fedha.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kuboresha miundombinu ya barabara nchini ili kurahisisha usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi.
Alitaja miradi ya ujenzi wa barabara za lami ya mkoani Mara iliyo kwenye orodha ya kukwamuliwa kuwa ni pamoja na ile ya Tarime-Mogabiri, Tarime-Mugumu na Sanzate-Natta.
“Hakutakuwa na ucheleweshaji wa fedha kwenda kwenye miradi hii, ili wananchi wa Mara wawe na miundombinu rafiki, wasikwame katika shughuli za uzalishaji,” alisema Dkt. Mwigulu.

No comments:
Post a Comment