NEWS

Wednesday, 15 July 2026

Dhahabu ya bilioni 1.3/- yakamatwa ikitoroshwa



Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa

Na Mwandishi Wetu,
Geita
--------------------------------------------------

Dhahabu yenye thamani ya shilingi zaidi ya bilioni 1.3 iliyokuwa ikitoroshwa kwenda nje ya nchi, imekamatwa na serikali mapema mwezi huu, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa.

Kukamatwa kwa dhahabu hiyo kunafuatia operesheni kali iliyoendeshwa na Tume ya Madini kwa kushirikiana na Kikosi Kazi cha Kuzuia Utoroshaji Madini pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Dkt. Kiruswa aliwambia waandishi wa habari mkoani Kagera juzi kuwa operesheni hiyo ilifanyika Julai 1, 2026, ambapo vipande 163 vya dhahabu yenye uzito wa gramu 4,434.66 na thamani ya shilingi 1,345,998,291.67 vilikamatwa vikisafirishwa kinyume cha sheria.

Alisema kukamatwa kwa dhahabu hiyo ni sehemu ya jitihada zinazofanywa na serikali kudhibiti utoroshaji madini na kulinda rasilimali za taifa.

Alionya kuwa serikali iko chonjo kuwabaini watu na mitandao yote inayojihusisha na biashara haramu ya madini.

"Tutaendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini kwa kuhakikisha madini yanauzwa kupitia mfumo rasmi wa serikali," alisema Dkt. Kiruswa.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, kati ya Julai 2025 na Machi 2026, serikali ilikamata madini yenye thamani ya shilingi bilioni 3.31 katika matukio 55 yaliyorekodiwa nchini.

Dkt. Kiruswa alisema taratibu za kuyataifisha madini yaliyokamatwa zinaendelea kwa mujibu wa sheria ili yawe mali ya serikali.

Alitumia fursa hiyo pia kuwataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kutumia masoko rasmi na vituo vya ununuzi vilivyoanzishwa nchini ili biashara ifanyike kwa uwazi na kuimarisha mapato ya serikali.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages