
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, akimpongeza Massana Gibril Mwishawa baada ya kumwapisha kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika hafla iliyofajika makao makuu ya shirika hilo la umma jijini Arusha wiki iliyopita.
Na Mwandishi Wetu
--------------------------------------------------------
Massana Gibril Mwishawa anatajwa na wengi kuwa ni mtu mwenye upendo, mnyenyekevu na mtaalam mbobezi wa masuala ya uhifadhi na utalii.
Katika historia ya maisha yake ni vigumu kumtenganisha na tasnia ya uhifadhi wa wanyamapori kwa sababu tangu ujana wake amekulia katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Mwishawa ambaye ni msomi mwenye Shahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Maliasili, anaamini kwamba wanyamapori wakubwa na wadogo ni hazina kubwa kwa taifa, hivyo wanastahili kulindwa kwa hali na mali.
Mapema mwezi huu, Mwishawa aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Uteuzi wake umebeba matumaini siyo tu ya wafanyakazi wa TANAPA, bali pia kwa jamii zote zinazoishi kuzunguka hifadhi za taifa na wadau wote wa uhifadhi na utalii waliopo ndani na nje ya nchi.
Akizungumza kwa unyenyekevu mkubwa, Kamishna Mwishawa alimshukuru mtangulizi wake na kuwataka maafisa na askari wote kuendeleza moyo na utamaduni wa ushirikiano wa wafanyakazi wa TANAPA kutoa mapendekezo yanayohitajika ili kufikia malengo yaliyowekwa ya taasisi.
"Kuaminiwa kwangu na kupewa jukumu hili na Mhe. Rais kwa kiasi kikubwa kumetokana na mchango na mapendekezo ya mtangulizi wangu. Naahidi kuendeleza misingi aliyoiacha ya uwazi, uwajibikaji na ubunifu katika kuongoza TANAPA," alisema Mwishawa baada ya makabidhiano ya ofisi na mtangulizi wake, Mussa Nassoro Kuji, yaliyofanyika wiki iliyopita makao makuu ya TANAPA, jijini Arusha.
Julai 9, 2026, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, alimwapisha Mwishawa kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA na kumuelekeza kusimamia miundombinu ya hifadhi, kuvutia wawekezaji na kubuni bidhaa mpya za utalii.
Vilevile, alimwelekeza kusimamia mapato, kuimarisha uhusiano na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi bila kusahau nidhamu, uadilifu, weledi, ustawi wa watumishi na maslahi yao kwa wakati.
Kamishna Mwishawa alitumia nafasi hiyo pia kumshukuru Rais Samia kwa kumuamini na kumpa dhamana hiyo, na kuahidi kutekeleza majukumu yake kwa uzalendo, uadilifu, uwajibikaji, nidhamu na weledi akishirikiana na watumishi wenzake.
Alisisitiza kuwa hifadhi za taifa ni hazina kubwa ya kiikolojia, kiuchumi na kijamii zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika mapato ya serikali na miradi ya kimkakati kama uzalishaji wa umeme.
Kabla ya kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Mwishawa, ambaye ni mbobezi wa uhifadhi, ulinzi mkakati wa maliasili na utalii, alikuwa Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara wa shirika hila la umma.
Akizungumza katika hafla hiyo ya uapisho wa Kamishna Mwishawa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Mkuu wa Majeshi (Mstaafu) Jenerali George Waitara.
Jenerali Waitara alisema bodi hiyo itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati na ushauri wakati wote ili kufanikisha adhma ya kuendeleza sekta ya maliasili na utalii.
Aidha, alisisitiza uendeshaji wa shughuli za TANAPA kwa uwazi na utoaji wa mrejesho uwahusishe maafisa na askari ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Hafla ya uapisho wa Kamishna Mwishawa ilihudhuriwa pia na wakuu wa taasisi za uhifadhi ikiwemo NCAA, TFS na wawakilishi wa TAWA, viongozi wa serikali, wadau wa uhifadhi na utalii, viongozi wa dini, Maafisa na Askari wa TANAPA.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment