NEWS

Sunday, 12 July 2026

Serikali kufanya maboresho makubwa ya miundombinu ya huduma za kijamii Butiama kumuenzi Mwalimu Nyerere



Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Mwigulu Nchemba (aliyevaa skafu), akisalimiana na Madaraka Nyerere, mmoja wa watoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipofanya ziara Butiama hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu
Butiama
--------------

Serikali imeahidi kufanya maboresho makubwa katika wilaya ya Butiama mkoani Mara, ikiwa ni hatua ya makusudi ya kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Wilaya hiyo ndiyo iliyorithi jina la kijiji cha Butiama, mahali alipozaliwa Mwalimu Nyerere mwaka 1922.

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye hivi karibuni alifanya ziara ya siku nne Mara, aliziagiza TARURA na Wizara ya Maji kuwasilisha tathmini katika kipindi cha mwezi mmoja kuhusu maboresho yanayohitajika ya upatikanaji maji na barabara, miongoni mwa miundombinu mingine muhimu katika wilaya hiyo.

Dkt. Nchemba aliwambia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mwenge kwamba amepokea maombi kutoka familia ya Baba wa Taifa ya maboresho ya miundombinu.

"Hili siyo upendeleo, bali Butiama inastahili kupewa kipaumbele kwa kuwa ni nyumbani kwa Baba wa Taifa, na hakuna Butiama nyingine," alisema Waziri Mkuu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, alisema Butiama ni wilaya ya kimkakati linapokuja suala la maendeleo.

Alisema kwa kuwa Butiama ni nyumbani kwa Baba wa Taifa, maboresho makubwa yakifanyika katika wilaya hiyo yatagusa mkoa wote wa Mara ambapo wilaya nyingine zote zinapakana na wilaya hiyo.

Mkoa wa Mara, ambao sasa unatimua mbio katika historia ya maendeleo ya Tanzania, una wilaya sita za Bunda, Butiama, Musoma, Rorya, Tarime na Serengeti.

Mkoa huo unajivunia Hifadhi maarufu duniani - Hifadhi ya Taifa Serengeti ambayo inahesabika kuwa sehemu ya urithi wa dunia.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages