NEWS

Friday, 3 July 2026

Waziri Mkuu: Serikali itaboresha Butiama kumuenzi Mwalimu Nyerere



Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (aliyevaa skafu) akisalimiana na Madaraka Nyerere ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wakati wa ziara yake ya kikazi leo Julai 3, 2026.

Na Mwandishi Wetu
Butiama
-----------------

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema serikali itafanya maboresho makubwa katika wilaya ya Butiama kwa ajili ya kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hivyo, ameitaka TARURA na Wizara ya Maji kuwasilisha tathmini ndani ya mwezi mmoja kuhusu maboresho yanayohitajika ili kuboresha upatikanaji wa maji, barabara na miundombinu mingine katika wilaya hiyo.

Dkt. ametoa kauli hiyo leo Julai 3, 2026, wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mwenge, ambapo amesema amepokea maombi ya familia ya Baba wa Taifa kuhusiana na maboresho ya ujenzi wa miundombinu hiyo.

"Hili sio upendeleo, bali Butiama inastahili kupewa kipaumbele na serikali kwa kuwa ni nyumbani kwa Baba wa Taifa," amesema Waziri Mkuu Mwigulu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, amesema Butiama ni wilaya ya kimkakati, hivyo maboresho makubwa yakifanyika yatagusa mkoa mzima wa Mara.

Awali, Dkt. Mwigulu amezuru na kuweka shada la maua katika Kaburi la Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambapo amepokewa na mtoto wa Mwalimu Nyerere, Madaraka Nyerere.

Waziri Mkuu Mwigulu akiweka shada la maua kwenye kaburi la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Mwitongo wilayani Butiama.

Waziri Mkuu huyo yuko mkoani Mara tangu juzi kwa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages