NEWS

Thursday, 9 July 2026

Mwishawa rasmi Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Waziri Kijaji ampa maelekezo kustawisha uhifadhi, utalii



Massana Gibril Mwishawa akila kiapo cha Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA jijini Arusha leo.

Na Calvin Katera
Arusha
--------------

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amemwelekeza Kamishna mpya wa Uhifadhi wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Gibril Mwishawa, kusimamia miundombinu ya hifadhi, kuvutia wawekezaji na kubuni bidhaa mpya za utalii.

Vilevile, amemwelekeza kusimamia mapato, kuimarisha uhusiano na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi bila kusahau nidhamu, uadilifu, weledi, ustawi wa watumishi na maslahi yao kwa wakati.

Waziri Kijaji ametoa maelekezo hayo leo Julai 9, 2026, jijini Arusha katika hafla ya uapisho wa Kamishna wa Uhifadhi Mwishawa ambaye aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuchukua nafasi ya Musa Nassoro Kuji aliyemaliza muda wake.

Waziri Kijaji akimpongeza Kamishna wa Uhifadhi Mwishawa

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Mkuu wa Majeshi (Mstaafu) Jenerali George Waitara, amesema bodi hiyo itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati na ushauri wakati wote ili kufanikisha adhma ya kuendeleza sekta ya maliasili na utalii.

Pia, amesisitiza uendeshaji wa shughuli za TANAPA kwa uwazi na utoaji wa mrejesho uwahusishe maafisa na askari ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi Mwishawa amesema Hifadhi za Taifa ni hazina kubwa ya kiikolojia, kiuchumi na kijamii zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika mapato ya serikali na miradi ya kimkakati kama uzalishaji wa umeme.

Kamishna Mwishawa ametumia nafasi hiyo pia kumshukuru Rais Samia kwa kumuamini na kumpa dhamana hiyo, na kuahidi kutekeleza majukumu yake kwa uzalendo, uadilifu, uwajibikaji, nidhamu na weledi akishirikiana na watumishi wenzake.



Hafla hiyo imehudhuriwa na wakuu wa taasisi za uhifadhi ikiwemo NCAA, TFS na wawakilishi wa TAWA, viongozi wa serikali, wadau wa uhifadhi na utalii, viongozi wa dini, Maafisa na Askari wa TANAPA.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages