NEWS

Thursday, 9 July 2026

Sekondari za juu Tarime DC zapokea msaada wa vifaa vya TEHAMA kutoka kwa Eliakim Maswi, Soya One



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (aliyechomekea shati), akiwa na viongozi mbalimbali wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya TEHAMA vilivyotolewa na Eliakim Maswi na Soya One kwa shule za sekondari za juu leo.

Na Mwandishi Wetu/ 
Mara Online News
Tarime
---------------

Wadau wa maendeleo Eliakim Maswi na Soya One Limited wametoa msaada wa vifaa mbalimbali vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi katika shule zote nane za sekondari za juu (high schools) zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.

Shule hizo ni Manga, JK Nyerere, Magoto, Borega, Ingwe, Nyanungu, Inchungu na Nyasaricho, ambazo kila moja ilikabidhiwa photocopy machine, projector, laptop na Wi-Fi Router kwa ajili ya intaneti ya mitandao.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Juster Magabe, wamekabidhi vifaa hivyo kwa viongozi wa shule hizo katika hafla iliyofanyika kwenye ofisi za halmashauri hiyo leo Alhamisi.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Mkurugenzi Mtendaji, Solomon Shati na baadhi ya madiwani na watumishi wa halmashauri hiyo, Juster amewashukuru Maswi na Soya One, akisema vifaa hivyo vitakuwa chachu ya kuinua taalamu na ufaulu wa wanafunzi katika shule hizo.

“Tunawashukuru sana wadau wetu wa maendeleo Eliakim Maswi na Soya One kwa moyo wao wa upendo na kujitolewa… Tukiwainua wanafunzi wetu leo - tunatengeneza wataalamu na viongozi watakaoijenga Tanzania ya kesho,” amesema Juster ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyakonga.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Manga, Mwalimu Editha Lazaro Nakei, naye amewashukuru wadau hao akisema vifaa hivyo vitakuwa hazina kwa matumizi ya TEHAMA yenye tija katika shule hizo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele, amesema Eliakim Maswi na Soya One ni wadau wa maendeleo wa muda wote wanaoonesha uzalendo na dhamira ya dhati ya kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha huduma za kijamii ikiwemo elimu.

“Sisi kama serikali tunawashukuru sana Eliakim Maswi na Soya One, hivi vifaaa walivyotoa vitunzwe kwa uzalendo mkubwa kama walivyovitoa kwa uzalendo,” amesema Meja Gowele ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya makabidhiano hayo.

Awali, Mkurugenzi wa Kampuni ya Soya One Limited yenye kaulimbiu ya “Jamii Kwanza”, Chacha Soya, amesema yeye na Maswi wanaona fahari kubwa kurudisha sehemu ya mapoto yao kwa jamii.

Soya ametumia nafasi hiyo pia kuwaomba walimu kuwapa wanafunzi ushirikiano mzuri katika matumizi ya vifaa hivyo kwa ufanisi ili kuwajengea uwezo wa kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia.

Eliakim Maswi ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watu wenye Mahitaji Maalum, amewakilishwa na mdau wa maendeleo mwenzake, Chacha Soya, katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages