
Prof. Sospeter Muhongo
Na Mwandishi Wetu
---------------------------
Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa 16 wa Akademia ya Sayansi ya Afrika (AAS) utakaofanyika jijini Dar es Salaam, Desemba 15 hadi 17, mwaka huu.
Mkutano huo utawaleta pamoja wanasayansi, watunga sera, washirika wa maendeleo, wenye viwanda, taasisi za fedha, mashirika na wawakilishi wa serikali kuzungumzia maendeleo ya sayansi, uimarishaji utafiti na uwekezaji katika sayansi, teknolojia na ubunifu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makamu wa Rais wa AAS wa eneo la nchi za Kanda ya Mashariki ya Afrika, Prof. Sospeter Muhongo, mada kuu ya mkutano huo itakuwa "Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Maendeleo Endelevu na Ustawi Kiuchumi Afrika".
Taarifa hiyo imesema nia kubwa ya mkutano huo, unaotarajiwa kufunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuvutia uwekezaji katika sayansi, ubadilishanaji maarifa, kujadili sera na kuimarisha ushirikishwaji katika utafiti.
Lengo kubwa la kuanzishwa kwa AAS ni kukuza na kuimarisha jamii ya kisayansi barani Afrika, hasa kwa wakati huu ambapo dunia inashuhudia maendeleo makubwa ya teknolojia katika kila nyanja ya kiuchumii na kijamii.
Taarifa ya Prof. Mujongo imeeleza kuwa mkutano huo umeandaliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana vyuo vikuu vya Dar es Salaam, Dodoma, Sokoine, Nelson Mandela na Suza.
Maandalizi ya mkutano yanafanywa na kamati mwenyeji ya hapa Tanzania ambayo inaongozwa na Prof. Muhongo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, mkoani Mara.
No comments:
Post a Comment