NEWS

Thursday, 23 July 2026

RC Mara: Tumefanikiwa mapambano dhidi ya kilimo cha bangi



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi (kulia), akizingumza na mgeni wake, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas James Lyimo, aliyemtembelea ofisini kwake mjini Musoma leo.

Na Mwandishi Wetu
Musoma
---------------

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, amesema kuna mabadiliko makubwa kwa wakazi wa mkoa huo ya kuchangamkia fursa halali za maendeleo zilizopo na kuachana na kilimo na biashara ya dawa za kulevya.

Kanali Mtambi ameyasema hayo leo Julai 23, 2026 alipompokea na kuzungumza na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas James Lyimo, ofisini kwa mjini Musoma.

“Kwa sasa wananchi wanajishughulisha zaidi na shughuli za kuwaletea maendeleo endelevu, ikiwemo uchimbaji wa madini, uvuvi, ufugaji wa samaki kwenye vizimba, kilimo na shughuli nyingine halali na hawahangaiki tena na kilimo cha bangi kama ilivyokuwa hapo awali,” amesema Kanali Mtambi.

Ameongeza kuwa wananchi wengi wameendelea kubadilika kwa kiwango kikubwa kutokana na ushirikiano uliopo kati ya serikali na wananchi katika kupambana na kilimo, biashara na matumizi ya dawa za kulevya, hususan bangi.

Kanali Mtambi amesema kuwa baada ya kudhibiti kilimo na biashara za dawa za kulevya, matukio ya uhalifu katika mkoa wa Mara kwa sasa yamepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya serikali na wananchi.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali Lyimo amesema mafanikio yaliyopatikana katika mkoa wa Mara yanadhihirisha ushirikiano mzuri uliopo baina ya DCEA, viongozi na wananchi wa mkoa huo.

Amefafanua kuwa kwa sasa takriban asilimia 80 ya wananchi wa mkoa huo wameachana na kilimo na biashara ya bangi kutokana na ushirikiano mkubwa kati ya mamlaka hiyo, viongozi na wananchi.

“Hapo zamani ilikuwa ni jambo la kawaida kukuta mashamba ya mahindi au mazao mengine yakiwa na bangi katika mkoa wa Mara, lakini kwa sasa kuna mabadiliko makubwa sana,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Kamishna huyo ametumia nafasi hiyo pia kupongeza hatua ya ushirikiano unaoendelea kutolewa kwa DCEA na viongozi wa mkoa wa Mara katika operesheni mbalimbali za kudhibiti dawa za kulevya, jambo ambalo amesema limesaidia kupungua athari za dawa za kulevya kwa maendeleo ya taifa na hususan kwa nguvukazi ya vijana na usalama wa rasilimali za nchi.

Amesema baadhi ya mataifa au makundi yenye maslahi hasi yanaweza kutumia dawa za kulevya kama njia ya kudhoofisha nguvukazi ya taifa na kupunguza uzalishaji na kwamba kama vijana wengi watakuwa wameathirika na dawa za kulevya inaweza kuhatarisha maendeleo na usalama wa taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages