NEWS

Saturday, 4 July 2026

Waziri Mkuu aipongeza Musoma Vijijini kwa usimamizi wa miradi akizindua Shule ya Msingi Kasoma



Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba (aliyevaa skafu) baada ya kukata utepe kuashiria uzinduzi wa Shule ya Msingi Kasoma, Musoma Vijijini leo. Wengine ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi (wa pili kulia), Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (aliyevaa kofia) na Mbunge wa jimbo hilo, Prof. Sospeter Muhongo (wa tatu kushoto), miongoni mwa viongozi wengine.

Na Mwandishi Wetu
Musoma
---------------

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameizindua Shule ya Msingi Kasoma katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, mkoani Mara na kuipongeza halmashauri hiyo kwa kusimamia miradi ya maendeleo kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Akizungumza baada ya kuzindua shule hiyo leo Julai 4, 2026, Dkt. Mwigulu alisema serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuhakikisha watoto wengi zaidi wanapata fursa ya kusoma katika mazingira bora na karibu na makazi yao.

"Nimeona usimamizi mzuri wa miradi unaozingatia thamani ya fedha. Hicho ndicho ambacho Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekikusudia kiwafikie wananchi. Hongereni sana," alisema.

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Musoma imeanza mapema kutekeleza mwelekeo wa serikali wa kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na shule ya sekondari, hatua ambayo itawezesha utekelezaji wa sera ya elimu ya lazima kwa miaka 10 kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne.

"Tulipanga ifikapo mwaka 2028 tuanze utekelezaji wa mfumo huu, lakini ninyi tayari mmeanza. Hongereni sana kwa hatua hiyo," alisema Waziri Mkuu Mwigulu.

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu (kulia) na Mbunge Prof. Muhongo wakipongezana wakati wa uzinduzi wa Shule ya Msingi Kasoma.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, alisema uwekezaji unaofanywa na serikali katika sekta ya elimu umeiwezesha wilaya hiyo kuendelea kupanua miundombinu ya shule ili kuendana na sera ya elimu ya lazima kwa miaka 10.

Prof. Muhongo alisema jimbo hilo lina shule za msingi 120, linaendelea kujenga shule nne mpya na tayari lina shule za sekondari 33 katika kata 21, lengo likiwa ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na shule ya sekondari sambamba na kuongeza idadi ya shule za sekondari za juu (High Schools).

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Msongela Palela, alisema mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Kasoma ulipokea shilingi milioni 330.7 kutoka Serikali Kuu kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST).

Kwa upande wake halmashauri hiyo ilichangia shilingi milioni 5.4 kwa ajili ya ununuzi wa madawati 90, huku wananchi wa kijiji cha Kaboni wakichangia nguvu kazi yenye thamani ya shilingi 800,000.

Msongela alisema mradi huo umejumuisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya elimu ya awali, madarasa sita ya shule ya msingi, jengo la utawala na vyoo.

Ujenzi wa shule hiyo alisema umeondoa kero wanafunzi kutembea umbali wa kilomita zaidi ya nne kufuata masomo, lakini pia umekiwezesha kijiji cha Kaboni kupata shule yake ya kwanza ya msingi na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages