NEWS

Tuesday, 7 July 2026

Waziri Mkuu Mwigulu awakaribisha wafanyabiashara wa Ufaransa kuwekeza viwanda vya kuongeza thamani madini Tanzania



Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza katika mkutano wa wafanyabiashara nchini Ufaransa jana.

Paris, Ufaransa

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewakaribisha wafanyabiashara wa Ufaransa kuja kuwekeza kwenye uongezaji thamani madini ya mkakati nchini Tanzania kwa kujenga viwanda vya kuchenjua, kusafisha na kuyeyusha madini.

Dkt. Mwigulu aliyasema hayo jana Julai 6, 2026 jijini Paris, Ufaransa wakati wa mkutano wa kibiashara baina ya sekta binafsi za Ufaransa na Tanzania wenye lengo la kubainisha fursa za kiuchumi na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

“Tanzania imebarikiwa kuwa na madini mengi yakiwemo madini ya kimkakati ambayo leo dunia inayahitaji sana, ni wakati muafaka kufikiria ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani madini katika eneo ambalo una uhakika wa malighafi ya kutosha.

“Nawakaribisha kuja kuwekeza Tanzania, nchi yenye sera zinazotabirika, vivutio vizuri vya uwekezaji na mazingira rafiki ya kufanya biashara ambayo yamesimamiwa vyema kwa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu. Hassan,” alisema Waziri Mkuu Mwigulu.

Naye Waziri wa Madini Tanzania, Anthony Mavunde, alisema uongezaji thamani madini ni takwa muhimu la Sera ya Madini na kwamba serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya kiuwekezaji ili kuvutia uwekezaji mkubwa kwenye kusafisha, kuchakata na kuyeyusha madini ndani ya nchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wafanyabiashara wa Tanzania na Ufaransa katika kusaidia kuongeza ujuzi, matumizi sahihi ya teknolojia na kukuza mitaji ili kufanya biashara kwa urahisi.

Picha ya pamoja

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages