NEWS

Friday, 3 July 2026

Rorya: Waziri Mkuu atoa mwezi mmoja mgao wa maji uishe Shirati



Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (aliyevaa skafu) akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Rorya jana. (Picha na Mara Online News)

Na Godfrey Marwa,
Rorya
--------------

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Lameck Mwigulu Nchemba, ametoa muda wa mwezi mmoja kwa mamlaka husika kuhakikisha mgao wa maji unaisha katika mjini Shirati wilayani Rorya, Mara.

Alitoa agizo hilo jana wakati akihutubia mkutano wa hadhara wilayani humo akisema ni aibu kuona wananchi hao wanaoishi jirani na Ziwa Victoria wakikosa maji.

Dkt. Mwigulu alitoa maelekezo hayo baada ya kutembelea daraja la mto Nyathorogo linalounganisha wilaya za Rorya na Tarime, lililojengwa kwa mawe kwa gharama ya shilingi milioni zaidi ya 700.

"Ndani ya mwezi mmoja wananchi wapate maji, sasa hivi fedha za maji zitaenda kwenye mfuko wake wa maji moja kwa moja. Ni aibu wananchi ambao wanaweza kufuata maji kwa ndoo ziwani kuwa na mgao wa maji,” alisema.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Mathew Kundo, alisema wao kama wizara hawatakuwa kikwazo na wapo tayari kushirikiana na viongozi wa Rorya kuhakikisha wananchi wanapata majisafi na salama.

"Mhe. Rais Dkt. Samia [Samia Suluhu Hassan] alishatoa maelekezo… nimemuelekeza Katibu Mkuu atume timu yake hapa Rorya kuhakikisha mgao wa maji unamalizwa. Wizara ya maji hatutakuwa kikwazo tunaenda kutatua changamoto hii,” alisema Mhandisi Kundo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu amesema kukwama kwa ujenzi wa barabara ya Utegi-Shirati kulitokana na uamuzi wa serikali wa kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya kimkakati, ukiwemo wa Bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere.

Hivyo, aliielekeza Wizara ya Ujenzi kutangaza tenda upya ndani ya mwezi mmoja ili ujenzi wa barabara hiyo uanze mara moja

Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, akitoa ufafanuzi kuhusu barabara hiyo alisema: "Mkandarasi aliyepewa kazi hiyo aliomba gharama kubwa hadi kufikia bilioni 126 na milioni 800 kwa kilomita 27, serikali ikakataa, hivyo ndani ya mwezi mmoja tutangaza tenda upya ya barabara hiyo ya Utegi-Shirati mpaka Kirongwe na pia Kuruya kwenda Kinesi.”

Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege, aliishukuru serikali na kusema kukamilika kwa daraja la mto Nyathorogo kutakuwa mkombozi wa uchumi wa Rorya.

Dkt. Mwigulu yuko mkoani Mara kwa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages