
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, akizungumza katika Mahafali ya 14 ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi, jijini Dar es Salaam jana.
Dar es Salaam
--------------------
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, jana Julai 23, 2026, alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mahafali ya 14 ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), yaliyofanyika Kunduchi jijini Dar es Salaam.
Mahafali hayo yalihitimisha mafunzo ya ngazi ya juu ya Mkakati wa Ulinzi na Usalama, ambapo wanafunzi 72 kutoka Tanzania na nchi mbalimbali walihitimu mafunzo hayo.
Akizungumza kwa niaba ya Rais katika hafla hiyo, Dkt. Nyansaho alisisitiza kuwa ulinzi na usalama wa taifa ni jukumu la kila Mtanzania, bila kujali nafasi au wajibu alionao.

Waziri Nyansaho alibainisha kuwa amani, utulivu na usalama wa nchi vinategemea ushirikiano wa wananchi wote katika kulinda mipaka, rasilimali na maslahi ya taifa.
Aidha, aliwataka wahitimu wa kozi hiyo kutumia maarifa, ujuzi na uzoefu walioupata katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na usalama katika maeneo yao ya kazi, huku wakisimamia kwa weledi na uzalendo ulinzi wa rasilimali na maslahi ya taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

No comments:
Post a Comment