NEWS

Tuesday, 25 August 2026

Makamu wa Rais Dkt. Nchimbi atangaza kujiuzulu



Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi

Na Mwandishi Wetu

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, leo Jumanne, Agosti 25, 2026 ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo na utumishi wa umma, kwa mujibu wa barua iliyosambaa katika mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa barua hiyo, uamuzi huo wa Dkt. Nchimbi utaanza kutekelezwa Septemba 4, 2026.

Katika barua aliyomwandikia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Nchimbi amesema amejiridhisha kuwa Rais Samia anatamani mabadiliko, hivyo ameona aachie ngazi kutimiza ahadi yake kwake.

Agosti 25, 2025, baada ya kuthibitishwa na Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Nchimbi alimuahidi Rais Samia kuwa siku yoyote atakayohitaji kuwa na Makamu wa Rais mwingine, yeye atakuwa tayari kuachia nafasi hiyo.

Dkt. Nchimbi ni mzoefu wa siasa za Tanzania baada ya kupitia kwenye mfumo wa uongozi wa chama hicho tawala kwenye Jumuiya ya Vijana na hatimaye kushika nyadhifa mbalimbali za kitaifa, zikiwemo uwaziri na ubalozi.

Kujiuzulu kwa kiongozi huyo huenda kukaleta mabadiliko makubwa serikalini, hasa madai yanayoendelea nchini ya kutaka iandikwe Katiba Mpya inayoendana na mazingira ya sasa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Dkt. Nchimbi amehudumu kama Makamu wa Rais kwa chini ya mwaka mmoja, tangu alipoapishwa kushika nafasi hiyo Novemba 5, 2025. Alimrithi Dkt. Philip Isdor Mpango, aliyekuwa Makamu wa Rais kati ya mwaka 2021 na 2025.

Hadi Mara Online News inachapisha habari hii, hakuna kauli yoyote iliyokuwa imetolewa na serikali kuhusu kujiuzulu kwa Dkt. Nchimbi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages