NEWS

Friday, 14 August 2026

Waziri Bashiru asisitiza mazingira bora ya elimu akizindua vyumba vya madarasa Serengeti



Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, akizindua vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Igina, Agosti 13, 2026. Aliyevaa nguo za kijani na njano ni Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mary Daniel Surati.

Na Mwandishi Wetu
Serengeti
--------------

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amezitaka halmashauri zote nchini kuwa na mpango mkakati wa kuhakikisha shule zote zinakuwa na miundombinu inayohitajika ili kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji.

Waziri Bashiru aliyasema hayo Agosti 13, 2026 wakati akizindua vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Igina iliyopo kata ta Matare katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 50 za mapato ya ndani ya halmashgauri hiyo.

Waziri Bashiru ambaye kitaaluma pia ni mwalimu, akionesha umahiri wake wa kuandika ubaoni.

"Ili kuhakikisha kwamba hatuna uhaba wa matundu ya vyoo na madawati kupindukia, tupange mipango yetu vizuri, tuhakikishe hatufanyi mambo kwa dharura dharura, tuwe na mkakati wa kimkoa na halmashauri,” alielekeza.

"Mimi ni mwalimu kitaaluma, maadui watatu kwa binadamu ni ujinga, marardhi na umaskini, ila ‘kamanda’ wa hayo ni ujinga. Matatizo yote yanayomkabili binadamu chanzo ni ujinga, na suluhisho ni elimu.

“Walimu hongereni sana, najua mzigo mlionao walimu kwa kazi kubwa mnayofanya, hii ni kazi takatifu, tunzeni haya majengo. Lazima tulinde mazingira na usalama wa watoto na walimu,” alisema.

Waziri Bashiru akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa madarasa hayo

Kuhusu walimu, Waziri Bashiru alisema serikali inaendelea kuongeza ajira ili kukabiliana na upungufu uliopo maeneo mengi nchini.

Alitumia nafasi hiyo pia kuwasilisha salamu za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wana-Serengeti, akisema “Rais anachoomba Watanzania muendelee kumuunga mkono kwa kuimarisha na kudumisha misingi aliyoanzisha baba wa taifa, ikiwemo kulinda na kudumisha umoja, mshikamano na amani.”

Nayo Taasisi ya Nyansaho (Nyansaho Foundation) kupitia kwa Mratibu wake wa Kanda ya Ziwa, Modester Mwema, iliahidi kuipatia shule ya Msingi Igina msaada wa madawati yenye dhamani ya shilingi milioni 1.2.
Modester alisema lengo ni kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Katika hafla hiyo ya uzinduzi wa madarasa hayo, Waziri Bashiru aliambatana na Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Gowele na Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mary Daniel Surati, miongoni mwa viongozi wengine wa chama na serikali.

Waziri Bashiru akisalimiana na wanafunzi wa Shule ya Msingi Igina. Aliyeweka mikono tumboni ni Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Gowele, na aliye nyuma yake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages