NEWS

Saturday, 22 August 2026

Mara: Harambee ya ujenzi bweni la wasichana yavuka lengo



Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete na mume wake, Marwa Mathayo wakizungumza katika Bima ya Afya kwa Wote na harambee ya ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike, lililofanyika CMG Hotels mjini Tarime jana Ijumaa.

Na Godfrey Marwa
Tarime
------------

Shilingi milioni 102.4 zimepatikana katika harambee ya kuchangia ujenzi wa bweni la kisasa la wanafunzi wa kike katika moja ya shule za sekondari mkaoni Mara.

Harambee hiyo ambayo iliandaliwa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete (CCM), ilifanyika jana Ijumaa katika ukumbi wa CMG Hotels mjini Tarime.

Tukio hilo lilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo, wakiwemo wabunge, viongozi wa chama na serikali wakingozwa na Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Kwa mujibu wa Kanali Mtambi, lengo la harambee hiyo lilikuwa kupata shilingi milioni 100, lakini imevuka lengo kwa asilimia 2.4, ambapo fedha taslimu ni shilingi milioni 81.6 na ahadi shilingi milioni 20.8.

"Kwa hiyo, nitaamua hilo bweni lijengwe jimbo gani ndani ya mkoa wa Mara,” alisema Kanali Mtambi.

Sehemu ya washiriki wakishangilia tukio katika harambee hiyo

Awali, Mbunge Ghati alisema lengo la kuandaa harambee hiyo ni kuinua kiwango cha elimu na kusaidia wasichana kutimiza ndoto zao za kupata elimu.

Wachangiaji katika harambee hiyo na kiasi walichotoa kikiwa kwenye mabano ni Mbunge Ghati (shilingi milioni 10), Kanali Mtambi (saruji mifuko 300) na Nyansaho Foundation (shilingi milioni 10).
Mratibu wa Nyansaho Foundation Kanda ya Ziwa, Modester Mwema, akikabidhi mchango wake kwa mgeni rasmi.

Wachangiaji wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dkt. Rhimo Nyansaho (shilingi milioni 10), Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo (shilingi milioni nne) na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafiz Amir (shilingi milioni tano).

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowelle (shilingi milioni mbili) Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dkt. Khalfan Haule (shilingi milioni moja) na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara (shilingi milioni mbili), miongoni mwa wachangiaji wengine.
Mbunge Waitara (aliyevaa kofia) na Mbunge Ghati (katikati), miongoni mwa viongozi wengine wakimpokea Kanali Mtambi katika viwanja vya CMG Hotels.

Mapema kabla ya harambee, Mbunge Ghati aliendesha kongamano maalum la elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote unaotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mbunge huyo aliunga mkono mpango huo wa serikali kwa kuzilipia kaya 20 zenye watu 120 zinazoishi katika mazingira magumu kifurushi cha bima hiyo.

"Mimi niliyeitisha kongamano hili nalisindikiza kwa kusaidia kaya 20 zenye jumla ya watu 120 wasio na uwezo wa kukata bima ili waweze kupata bima hiyo," alisema Ghati.

Kanali Mtambi alimpongeza Mbunge Ghati kwa kuandaa kongamano hilo na kutoa wito kwa watu wote kusambaza elimu hiyo kwa jamii wanazotoka.

"Hongera sana kwa kuleta kongamano hili la bima ya afya kwa wote, watu leo wamepata elimu. Nnitoe wito mkawe mabalozi wazuri kwa kutoa taarifa sahihi juu ya mfuko huu wa Bima ya Afya kwa Wote," alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages