NEWS

Friday, 21 August 2026

Watoto zaidi ya milioni moja wenye umri chini ya miaka 10 kupewa chanjo ya polio Mara



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (katikati waliokaa), katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali serikali, wakiwemo wakuu wa wilaya wakati wa kikao kilichoangazia maandalizi ya chanjo ya polio kwa watoto kilichofanyika mjini Musoma jana Alhamisi.

Na Mwandishi Wetu
Musoma
--------------

Watoto zaidi ya milioni moja wenye umri chini ya miaka 10 wanatarajiwa kupewa chanjo ya polio (ugonjwa wa kupooza) katika mkoa wa Mara.

Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dkt. Zabron Masatu, katika kikao cha Mkuu wa Mkoa na maafisa wa serikali kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI na wakuu wa wilaya, miongoni mwa wengine.

Kikao hicho kilifanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara mjini Musoma jana Alhamisi, ambapo Dkt. Masatu alisema chanjo hiyo itatolewa kuanzia Agosti 27 hadi 30, 2026.

Dkt. Masatu alisema lengo la chanjo hiyo ni kuwakinga watoto hao dhidi ya virusi vya ugonjwa wa polio unaotajwa kusababisha ulemavu wa kudumu na hata vifo.

“Utoaji wa dawa hizo ni kinga kwa watoto dhidi ya ugonjwa hatari wa polio ambao kwa kiasi kikubwa hauna tiba,” alisema.

Naye Dkt. Joseph Mdachi kutoka Mapango wa Taifa wa Chanjo unaotekelezwa chini ya Wizara ya Afya, alisema serikali inatoa chanjo hiyo ili kuhakikisha watoto wote wa Kundi lengwa wanalindwa dhidi ya polio.

Dkt. Mdachi alieleza kuwa chanjo ya polio ni salama na yenye ufanisi mkubwa katika kuzuia ulemavu wa kudumu na hata vifo vinavyoweza kusababishwa na ugonjwa huo hatari.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, aliwaagiza wakuu wa wilaya kusimamia utoaji wa chanjo hiyo katika halmashauri zote za mkoa huo unafanyika kwa ufanisi.

Aidha, Kanali Mtambi aliwataka wazazi, walezi na wana-Mara kwa ujumla kuwapa wataalamu wa afya ushirikiano kwa kutoa taarifa sahihi na kuhakikisha kila mtoto aliye katika kundi lengwa anapata chanjo hiyo muhimu.

Tayari wataalamu kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo, Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) wapo mkoani Mara kwa maandalizi ya utoaji wa chanjo hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages