NEWS

Sunday, 16 August 2026

Nyamongo: CSR Barrick yawezesha ujenzi jengo la utawala Sekondari ya Mjini Kati



Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa pili kulia), akifurahi kuzindua mradi wa jengo la utawala la Shule ya Sekondari Mjini Kati uliotekelezwa chini ya CSR Barrick North Mara. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, miongoni mwa viongozi wengine.

Na Mwandishi Wetu,
Tarime
------------

Walimu waliokuwa wakilazimika kutumia vyumba vya madarasa kama ofisi katika Shule ya Sekondari Mjini Kati iliyopo Nyamongo wilayani Tarime, sasa wanafurahi kupata jengo jipya la utawala kutokana na mwendelezo wa utekelezaji wa mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Mgodi huo ambao unaendeshwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals, umetumia shilingi milioni 172 kugharimia utekelezaji wa mradi huo ili kuleta ahueni kwa walimu wa shule hiyo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, alizindua mradi huo wakati wa zaira yake ya kikazi mkoani Mara, Agosti 14, 2026.

“Lengo la mradi huu ni kuboresha mazingira ya kiutawala, kujifunzia na kufundishia kwa walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mjini Kati. Kabla ya mradi huu, walimu walikuwa wanatumia vyumba vya madarasa kama jengo la utawala,” ilieleza sehemu ya taarifa iliyosomwa na Kaimu Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Charles Gibiti Pius, kwa Waziri Bashiru.

Walimu wa shule hiyo waliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakisema mradi huo umesaidia kuamsha morali na ari ya ufundishaji kwa walimu.

Waziri Bashiru akiongozwa na Mwalimu Gibiti kukagua jengo hilo

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Waziri Bashiru aliuagiza uongozi wa wilaya na halmashauri kuhakikisha jengo hilo la utawala linawekewa samani na huduma za umeme na maji ili kuwezesha walimu kutekeleza majikumu ya kiutawala kwa ufanisi.

"Jengo tunalozindua halina samani DC (Mkuu wa Wilaya) jadilianeni na halmashauri, naomba kama Mlezi wa Mkoa [wa Mara], nilichokizundua jipekue muweke maji, samani na umeme, popote nilipozindua yanayotakiwa kukamilishwa yakamilishwe,” aliagiza.

Sehemu ya viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Mgodi wa North Mara walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa jengo hilo.

Mjini Kati ni moja ya shule za sekondari 53 za serikali zilizopo katika Hamashauri ya Wilaya ya Tarime.

Sekta ya elimu inatajwa kuchukua sehemu kubwa ya mabilioni ya fedha za CSR yanayotolewa na kampuni ya Barrick kufadhili miradi ya endelevu ya maendeleo ya jamii katika halmashauri hiyo.

Miradi inayotekelezwa kwa kutumia fedha za CSR kutoka mgodi huo inahusisha pia ujenzi wa nyumba za walimu, utengenezaji wa madawati kwa shule za msingi, viti na meza kwa shule za sekondari.

Mapema mwezi huu, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, alizindua pia vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari Matongo ambavyo pia vimejengwa kutokana na fedha za CSR Barrick North Mara.

Miradi hiyo ni sehemu ya miradi mipya 103 ambayo inatekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime chini ya mpango wa CSR Barrick North Mara.

Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa Mgodi wa North Mara umetumia shilingi bilioni 26.86 kugharimia utekelezaji wa miradi ya CSR 255 katika sekta za elimu, afya, barabara, maji, miradi ya kiuchumi na mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime tangu mwaka 2019 ulipokabidhiwa kwa Barrick.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages