
Kutoka kushoto ni Prof. Sospeter Muhongo, Dkt. Medard Kalemani na January Makamba wakiwa kwenye sherehe ya uzinduzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) mkoani Pwani jana Agosti 22, 2026.
Pwani
------------
Mawaziri watano walioshiriki kwa nyakati tofauti katika upangaji na utekelezaji wa Mradi wa Kufua Umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), ni miongoni mwa waalikwa muhimu waliohudhuria uzinduzi wa mradi huo.
Watano hao ni Prof. Sospeter Muhongo, Dkt. Medard Kalemani, January Makamba, Dkt. Doto Biteko na Deogratius Ndejembi ambaye ni Waziri wa Nishati wa sasa.
Mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha umeme megawati 2,115 ulizinduliwa rasmi jana Agosti 22, 2026 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Uzinduzi huo umeashiria kilele cha safari ya muda mrefu ya taifa katika kutekeleza mradi mkubwa wa kimkakati wa kuzalisha umeme kutoka Mto Rufiji, eneo la Stiegler’s Gorge, mkoani Pwani.

Rais Samia akipokea zawadi ya kutambua mchango wake mkubwa kwenye ukamilishaji wa Mradi wa JNPP.
Utekelezaji wa mradi huo wenye thamani ya takriban shilingi trilioni 7.5 umegharimiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.
Serikali za awamu zote sita zilisimamia tafiti na maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo ambao ni maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere miaka ya 1970.
Mradi huo uliendelea kuratibiwa katika uongozi wa Rais Ali Hassan Mwinyi na Benjamin William Mkapa, kisha uongozi wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete uliendelea na tafiti, tathmini za mazingira na maandalizi.
Ujenzi wa mradi huo ulianza rasmi kwa kuwekwa Jiwe la Msingi, Julai 26, 2019 na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
No comments:
Post a Comment