
Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara.
Mara Online News
Tarime
-------------
Tarime
-------------
Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwita Waitara, ameibuka na tuhuma nzito dhidi ya kiongozi aliyemtaja kama mtendaji wa chama hicho ngazi ya wilaya, akidai anamtegea misumari na ‘shot’ ya kisiasa.
Kwamba kiongozi huyo anatekeleza ‘mradi’ wa kumchonganisha na viongozi wa kata, matawi na wanachama wa CCM kwa ujumla katika jimbo hilo kuelekea uchaguzi wa ndani wa chama hicho tawala unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Tarime juzi, Waitara alilalamika kwamba kitendo hicho kinatishia umoja na mshikamano wa viongozi na wanachama wa CCM katika wilaya ya Tarime.
Mbunge huyo alitoa madai hayo baada ya ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Fadhili Maganya, iliyofanyika mjini Tarime, ambapo viongozi na wanachama kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Tarime walihudhuria.
Alisema mamia ya wanachama wa CCM na wazee wa mila kutoka majimbo ya Tarime Vijijini na Tarime Mjini walihudhuria mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya CMG hivi karibuni.
Waitara alisema kwa kawaida ugeni wa kiongozi wa ngazi ya taifa uliopangwa na uongozi wa wilaya, wajumbe wanaoalikwa wanapaswa kuwezeshwa kwa mahitaji muhimu, ikiwamo chakula, maji na nauli.
Alisema alitoa udhuru wa kutohudhuria mkutano huo, huku akiahidi kuchangia chochote kwa kadiri atakavyoweza.
Hata hivyo, alisema kilichomkwaza ni kupewa jukumu la kuwahudumia wajumbe 461 kutoka Tarime Vijijini dakika chache kabla ya mkutano huo kuanza.
“Zimebaki dakika tatu, ninapewa barua kwamba wajumbe wote kutoka Tarime Vijijini mimi ndiye nitawasimamia,” alisema Waitara, akieleza ukubwa wa gharama ambazo angehitajika kuzibeba ghafla.
“Wajumbe 461 ukiwapa shilingi elfu kumi kumi unazungumza milioni nne, laki sita na elfu kumi. Ukiwapa elfu ishirini ishirini unazungumza milioni zaidi ya tisa. Ukiwapa elfu thelathini thelathini unazungumza zaidi ya milioni 11, unaambiwa zimebaki dakika tatu,” alilalamika.
Mbunge huyo alisema alikuwa na wakati mugumu baada ya mgeni kuondoka, ambapo wajumbe kutoka Tarime Vijijini walielekezwa kwenda kwa katibu wake kwa ajili ya kupewa nauli, kitu ambacho alisema hakikuandaliwa.
Waitara alidai kuwa kitendo hicho kililenga kumweka katika mazingira ambayo wanachama wangemwona kama kiongozi aliyeshindwa kuwajibika kwa watu wake.
“Maana yake ni kwamba anataka wale wajumbe wakitoka wamchukie mbunge kwamba ameshindwa kusaidia watu wake,” alisema Waitara.
Waitara alienda mbali zaidi kwa kudai kuwa kuna watu wanaotamani kutumia mgogoro huo kama fursa ya kisiasa kuelekea uchaguzi wa viongozi wa CCM mwakani na Uchaguzi Mkuu mwaka 2030.
“Hivi ukianza kuwafanya wajumbe na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wasimwamini mbunge kuanzia leo mpaka 2030 itakuwaje katika hili jimbo?” alihoji.
Alidai kuwa baadhi ya watu waliowania ubunge wa jimbo la Tarime Vijijini mwaka 2025 bado wanaendelea kufanya shughuli za kisiasa ndani ya Tarime, akisema anahofu ya kuwepo kwa mpango wa kumdhoofisha kisiasa.
“Maana yake ni kwamba yeye [akitaja cheo cha kiongozi anayemtuhumu] na wenzake wapate mwanya sasa wa kutafuta watia nia ambao wapo already (tayari), ee wapo tayari hapa Tarime, waliokuwepo 2025 wapo mpaka leo na anafanya nao kazi,” alisema.
Hivyo, Waitara alisisitiza kuwa anachokiona katika sakata hilo ni uchonganishi unaoweza kuathiri mshikamano wa viongozi na wanachama wa CCM katika wilaya ya Tarime.
Alisema haiwezekani chama kikajenga umoja wakati baadhi ya viongozi wake wanatumia nafasi zao kuchonganisha wengine kwa wanachama. “Umoja hauwezi kuwepo kama tutakuwa tunapigana shot,” alisema.
Mbunge huyo alisema tayari amewasilisha malalamiko yake katika ngazi mbalimbali za chama, ikiwamo Kamati ya Siasa Mkoa wa Mara na ngazi ya taifa.
Kutokana na hali hiyo, alisema iwapo atachukua hatua za kutotoa ushirikiano kwa kiongozi anayemtuhumu, viongozi wengine wasimshangae.
“Siwezi kutoa ushirikiano kwa kiongozi ambaye yeye kazi yake ni kunitegea misumari, amenipiganisha muda mrefu… alinishughulikia kipindi kile na akatangaza mimi sitakiwi kuwa mbunge wa jimbo na akasema hanitambui,” alisema Waitara.
Alisisitiza kuwa umefika wakati ambao hawezi kuendelea kukaa kimya kuhusu kile anachodai kuwa ni mwenendo wa muda mrefu wa kiongozi huyo kutaka kumdhoofisha kisiasa.
Alisema ataandika malalamiko rasmi na kuyawasilisha kwa uongozi wa juu wa CCM na kwamba yuko tayari kufichua ‘figisu’ nyingine alizofanyiwa katika kipindi cha nyuma.
“Huu ni ugonjwa ambao haupaswi kulelewa, na hili jambo mimi nitaliandikia rasmi, sasa nitafukua makaburi yote ya mambo aliyonifanyia, hili jambo nimechoka na siwezi kulinyamazia.
“Kama hawawezi kuchukua hatua it is fine (sawa), mimi nitafanya kazi na wananchi, nitafanya kazi na viongozi ambao wananiheshimu na kutambua nafasi yangu, huo ndiyo msimamo wangu,” alisema Mbunge Waitara.
Mara Online News inaendelea na juhudi za kutafuta uongozi wa CCM Wilaya ya Tarime kwa ajili ya ufafanuzi wa suala hilo.
No comments:
Post a Comment