
Mbunge Mwita Waitara
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
-------------
Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, ameuliza swali bungeni akitaka kujua ni lini serikali itafanya utafiti wa madini katika vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti upande wa jimbo hilo, ili kuwezesha vijana wa maeneo hayo kunufaika kiuchumi.
Amesema kuna taarifa kwamba maeneo hayo yana madini, hivyo akataka serikali ifanye utafiti wa kitaalamu ili kubaini aina na kiwango cha madini yaliyopo na hatimaye kuwezesha wananchi, hususan vijana kuchimba na kunufaika na rasilimali hiyo.
“Kata za Kwihancha, Gorong’a na Nyanugu zina vijiji saba, inasemekana kuna madini pale, ningeomba nijue ni lini serikali itafanya utafiti kwenye maeneo yale vijana wapate nafasi ya kuchimba na kunufaika,” Waitara alihoji bungeni jijini Dodoma, jana Alhamisi, Agosti 26, 2026.
Kabla ya kuuliza swali hilo, mbunge huyo alimpongeza Waziri wa Madini kwa ahadi yake kwamba Agosti 31, 2026 wataalamu watakwenda Nyamongo jimboni humo na ndege nyuki (drone) kuangalia maeneo yanayoweza kufanyiwa utafiti kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini.
Akijibu swali la Waitara, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, naye alianza kwa kumpongeza mbunge huyo, akimtaja kama mtetezi wa kweli wa wachimbaji na msemaji mzuri katika sekta ya madini.
Dkt. Kiruswa alisema matumizi ya maeneo yaliyotengwa kisheria kwa madhumuni maalumu, kama vile hifadhi za wanyamapori na malisho ya mifugo yana taratibu za zinazopaswa kufuatwa kabla ya kubadilishiwa matumizi.
“Taratibu zinapozingatiwa kwa eneo ambalo lina manufaa makubwa ya kiuchumi na aina nyingine ya uwekezaji ambao una tija zaidi kwa taifa, kuna utaratibu wa kulitenga kwa ajili ya wachimbaji ambao wako tayari kuwekeza,” alisema.
Alitoa mfano wa madini ya urani yanayochimbwa katika eneo la Mto Mkuju, akieleza kuwa awali lilikuwa sehemu ya Pori la Akiba la Selous ambalo baadaye limekuwa sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.
Kwa mujibu wa Dkt. Kiruswa, uchimbaji wa urani katika eneo hilo umewezekana baada ya taratibu za kisheria kufuatwa na hatimaye kutengwa kwa ajili ya shughuli za uchimbaji wa madini hayo.
Akiizungumzia maeneo yaliyotajwa na Mbunge Waitara, Naibu Waziri Kiruswa alisema uwezekano wa kuyaidhinisha kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini upo iwapo taratibu zinazotakiwa kisheria zitazingatiwa na tathmini zinazohitajika kufanyika.
“Hivyo, katika eneo la Serengeti, taratibu hizo zikiweza kuzingatiwa na tathmini zikafanyika, uwezekano upo,” alisema Naibu Waziri Kiruswa.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya uwekezaji na uchumi, hatua hiyo itakuwa na umuhimu mkubwa kiuchumi kwa wananchi wa Tarime Vijijini, iwapo utafiti utathibitisha uwepo wa madini na serikali kuruhusu shughuli za uchimbaji bila kukiuka sheria za uhifadhi na ardhi.
No comments:
Post a Comment