
Rehema Juma Magawa na Izdory George Michael enzi za uhai
Pwani
-------------
Askari wa Jeshi la Polisi, Izdory George Michael na Rehema Juma Magawa, wamefariki dunia baada ya kugongwa na gari katika eneo la Maili Moja, wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.
Ajali hiyo ilitokea Agosti 25, 2026, saa 1:40 usiku wakati askari hao wakiwa eneo la kivuko cha watembea (zebra) kwa miguu katika barabara kuu ya Dar es Salaam–Morogoro.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T.804 ERM, lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Mlandizi, liliwagonga watembea kwa miguu katika eneo hilo.
Gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Josia Isaya Arute (34), mkazi wa Mlandizi.
Inadaiwa kuwa dereva huyo alipofika eneo hilo alikuta magari kadhaa yamesimama kusubiri watembea kwa miguu wavuke Barabara, lakini gari hilo liliyapita na kugonga watu kadhaa waliokuwa wakivuka, wakiwemo askari hao.
Miongoni mwa waliogongwa walikuwa askari wawili wa Polisi, Izdory George Michael na Rehema Juma Magawa.
Izdory alifariki dunia kwenye eneo la ajali wakati Rehema alipoteza uhai siku iliyofuata (Agosti 26, 2026) wakati akiendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Tumbi.
Baada ya ajali, dereva wa gari hilo aliondoka katika eneo la tukio, lakini Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi walifanya msako na kufanikiwa kulikamata gari hilo likiwa limefishwa katika eneo la Kwa Mfipa wilayani Kibaha.
Miili ya askari hao iliagwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Tumbi kabla ya kusafirishwa kwenda mikoani kwa ajili ya mazishi.
Ibada ya kuwaaga ilihudhuriwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi Salim Morcase, pamoja na askari wa vyeo mbalimbali, ndugu na waombolezaji wengine.
Mwili wa Rehema Juma Magawa ulipelekwa Korogwe mkoani Tanga, huku mwili wa Izdory George Michael ukisafirishwa kwenda Sumbawanga Vijijini mkoani Rukwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limeendelea kutoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuheshimu alama za barabarani, hususan maeneo ya vivuko vya watembea kwa miguu ili kuepusha ajali.
No comments:
Post a Comment