NEWS

Friday, 28 August 2026

Serikali yasisitiza kufufua Mnada wa Mifugo Magena



Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (katikati) akizungumza katika Mada wa Mifugo wa Kimataifa Magena hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
------------

Serikali imeendelea kuahidi kufufua Mnada wa Mifugo wa Kimataifa wa Magena ambao haufanyi kazi kwa miaka takriban 20 sasa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, alisisitiza ahadi hiyo hivi karibuni wakati alipotembelea mnada huo uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Tarime, mkoani Mara.

"Tunataka kufufua Mnada wa Magena. Kama Mratibu wa Shughuli za Maendeleo Mkoa wa Mara, nataka Mara iwe mfano wa kuigwa kwa ufugaji wa kisasa kwa kuwa na kituo cha kuzalisha mbegu bora za mifugo, na kuleta mafunzo, mbegu na utaalamu,” aliahidi Waziri Bashiru.

Taarifa za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zinaonesha kuwa katika mwaka wa fedha 2021/2022, serikali ilitumia shilingi milioni 175.65 kugharimia ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya mnada huo, ikiwemo mazizi, kipakilio, birika la maji na vyoo.

Wakati huo huo, Waziri Bashiru amepiga marufuku utoroshwaji wa mifugo kwenda nje ya nchi na kuvitaka vyombo vya usalama kushirikiana na viongozi wa wilaya, kata, vijiji na vitongoji kushirikiana kukomesha vitendo hivyo vya uhujumu uchumi.

"Naomba ushirikiano wa ulinzi na usalama ngazi zote, madiwani, uongozi wa vijiji na vitongoji tusiruhusu utoroshaji wa ajira na fedha za kigeni kutoka nchi yetu.

"Naomba tuache kuendesha sekta hizi kienyeji kwa mifumo isiyo rasmi, ujumbe ufike nchi nzima, nitawakamata kwa sababu sheria na vyombo vipo.

"DC (Mkuu wa Wilaya), niandalie makundi yote, nitakuja tuzungumze kuhusu ufugaji na uvuvi, naomba ushirikiano wa wafugaji, wavuvi na vyama vyao, wadau wakiwemo wafanyabiashara,” alisema Waziri Bashiru.

Awali, Mkuu wa huo, Issa Shabani, alimweleza Waziri Bashiru kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakitumia kigezo cha ukosefu wa soko kutorosha mifugo kwenda nje ya nchi.

"Mkoa wetu una vipenyo (njia zisizo rasmi) vingi sana vinapelekea utoroshwaji wa mifugo, ikiwemo siku za masoko kuingiliana na nchi jirani,” alisema.

Tarime inatajwa kuwa miongoni mwa wilaya zenye wazalishaji wakubwa wa mifugo katika Afrika Mashariki.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages