NEWS

Monday, 10 August 2026

Watu 14 wanaswa kwa tuhuma za utoroshaji madini



Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
--------------------

Watu 14 wamekamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya utoroshaji wa madini, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema.

Waziri Mavunde aliwambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaama jana kwamba kukamatwa kwa watu hao kumefuatia kugundulika kwa soko bubu la madini jijini Dar es Salaam.

Alisema watuhumiwa hao wamepanga nyumba Dar es Salaam na kuigeuza soko la madini kinyume cha sheria, licha ya serikali kuwezesha uwepo wa masoko na vituo vya ununuzi vilivyosambaa nchi nzima.

Waziri huyo alisema serikali itafanya ukaguzi maalum kwenye baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine kubaini nyumba zinazotumika kama masoko ya madini na chanzo cha utoroshaji wake.

Alisema taarifa za awali zinaonesha kuwa raia wa kigeni anahusika na biashara hiyo haramu ya utoroshaji madini nje ya mfumo rasmi na kwamba sasa amedhibitiwa.

Waziri Mavunde alivielekeza vyombo vya dola kuwabaini na kuwakamata wahusika wote kwenye mnyororo wa utotoshaji madini.

Alisema gramu 174 za madini yaliyokutwa katika soko bubu pamoja na mashine mbili za XRF aina ya NITON DXL 800, mizani ya kupimia uzito, mitungi ya gesi, vyungu vya kuchomea dhahabu, legis za kutengenezea umbo la dhahabu na shilingi milioni 54,705,000 vyote vinashikiliwa na serikali.

Serikali imekuwa ikiendesha msako mkali wa kimya kimya nchini kote kuwanasa watu wanaojihusisha na biashara ya madini nje ya mfumo rasmi, ikiwa ni hatua ya kulinda rasilimali za taifa dhidi ya aina yoyote ya uporaji.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages