
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akikata utepe kuzindua utafiti wa dhahabu kwa kutumia helikopta eneo la Nyamongo wilayani Tarime leo Agosti 31, 2026. Mwenye koti jeuzi ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi na katikati yao ni Meneja Mkazi wa Kampuni ya Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, miongoni mwa viongozi wengine.
Tarime
--------------
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amezindua utafiti wa dhahabu kwa kutumia helikopta ya Barrick kwenye maeneo yalioyo chini ya kampuni hiyo na wachimbaji wadogo katika wilaya ya Tarime mkoani Mara.
Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatatu, Agosti 31, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, uzinduzi wa utafiti huo ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuwezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika mnyoyoyo wa thamani ya madini.
Amesema utafiti huo wa kisayansi unatarajiwa kuleta neema kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu.
"Utafiti huu utawatoa (wachimbaji wadogo) kwenye uchimbaji wa kubahatisha," amesema Waziri huyo mwenye dhamana ya madini nchini.
Aliishukuru Kampuni ya Barrick nchini kwa kukubali ombi lake la kutaka helikopta hiyo kufanya utafiti kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo waliopewa leseni katika wilaya ya Tarime na maeneo jirani.
"Helikopta hii itaenda Majimoto (wilayani Serengeti) na maeneo mengine yenye leseni za uchimbaji za vijana. Niwashukuru sana ndugu zangu wa Barrick mkiongozwa na Dkt. Melkiory na Apolinary," amesema.

Helikopta ya utafiti huo wa dhahabu
Miongoni mwa maeneo ya leseni ambazo helikopta hiyo itafanya utafiti ni zile ambazo vijana takriban 200 walipewa na serikali, zikiwemo zilizorudishwa na Kampuni ya Barrick mwaka jana.
Helikopta hiyo ambayo itakuwa ikiruka umbali wa mita 30 kutoka uso wa dunia, ina vifaa vya kisasa vyenye uwezo wa kubaini miamba ya chini ya ardhi yenye uwezekano mkubwa wa kuwa na dhahabu ili kuruhusu hatua za tathmini na uchimbaji.
Uzinduzi wa utafiti huo umefanyika sambamba na uzinduzi wa Programu ya Madini kwa Kesho Njema (Mining for a Brighter Tomorrow – MBT), ambao umefanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Ingwe iliyopo Nyamongo.
Mavunde amesema walengwa wakuu programu ya MBT ambayo ni ya kitaifa, ni vijana, wanawake na watu wenye ulemavu nchini.

Waziri Mavunde na viongozi wengine mbalimbali wakifanya zoezi la kukimbia pamoja na vijana wachimbaji wadogo wa madini mjini Nyamongo leo.
Waziri Mavunde amesema uzinduzi wa mipango hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wizara yake ili kuhakikisha makundi hayo yananufaika na ukuaji wa sekta ya madini nchini.
"Haya ni matokeo ya maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan," amesema.
Aidha, Waziri Mavunde amesema ataendelea kuhakikisha kuwa migodi yote ya madini nchini inaongozwa na Watanzania ili kupunguza migogoro na jamii kama ilivyo kwa Kampuni ya Barrick.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyeki wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, amesema ujio wa utafiti wa madini kwa kutumia helikopta ni jambo la kujivunia.
"Tunapongeza Barrick kwa teknolojia hii,” amesema Mgalu huku akionesha matumani makubwa kuwa taarifa zitakazopatakina kutokana na utafiti huo zitafungua fursa zaidi katika kuinua uchumi wa Watanzania.
Aidha, Mgalu ameipongeza serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuzindua Programu ya MBT akisema ni hatua nzuri katika kuwezesha makundi lengwa. "Tunaipongeza serikali kwa hatua hii muhimu, kwa kweli hili ni jambo la kishitoria," amesema.
Kwa upande wake Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, amesema wameshiriki katika utekelezaji wa programu hiyo, ikiwa ni pamoja na kurudisha serikalini baadhi ya leseni zake za utafiti wa madini kwa ajili ya kunufaisha vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum.
"Sisi kama North Mara (Mgodi wa Barrick North Mara) tumerudisha leseni za utafiti 50 kwa vijana karibia 2,000," amesema Dkt. Ngido.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara na Mgodi wa Dhahabu wa Bylunhulu ambao upo wilayani Kahama, Shinyanga inaendeshwa na Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Dkt Ngido amesema migodi hiyo ina mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa huku akishukuru kwa ushirikiano mzuri ambao inapata kutoka serikalini.
"North Mara na Bulyanhulu ndio walipaji wakubwa wa kodi nchini na ndio migodi inayoongoza kwa kutoa gawio kubwa serikalini.
“Tutaendelea kushirikiana na serikali, wizara ya madini na jamii inayotuzunguka. Tunaleta maendeleo, tunatoa ajira na kukuza uchumi wa jamii," amesema Meneja Mkazi huyo wa Kampuni ya Barrick hapa Tanzania.
Kwa upande wake, Victor Tesha kutoka Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), amesema bado vijana wanahitaji vifaa vya utafiti na uchimbaji madini ulio salama.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi, ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuzindua utafiti wa dhahabu kwa kutumia helikopta na Programu ya MBT kitaifa mkoani Mara.
"Nashukuru kwa kuchagua Mara, tunaiona sayansi kwenye sekta ya madini," amesema RC Mtambi.
Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, naye ameishukuru serikali na Barrick kwa kuwezesha matukio ya kimaendeleo, ikiwemo ugawaji wa leseni kwa vikundi vya vijana wachimbaji wa madini katika eneo hilo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi, yeye amewapongeza wakazi wa Nyamongo kwa ushirikiano wao uliosaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa vitendo vya uvamizi dhidi ya mgodi wa Barrick North Mara.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Simon Sirro, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North, Apolinary Lyambiko, miongoni mwa viongozi wengine.
No comments:
Post a Comment