NEWS

Thursday, 17 September 2026

Air Tanzania yaanza kutua Musoma baada ya miaka 8



Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ikitua kwenye Uwanja wa Ndege Musoma mkoani Mara jana Alhamisi.

Na Godfrey Marwa
Musoma
--------------

Hatimaye ndege ya abiria ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ilianza kutua kwenye Uwanja wa Ndege Musoma mkoani Mara, ikitokea Dar es Salaam kupitia Mwanza jana Alhamisi.

Baadaye iliruka kwenda Dar es Salaam kupitia Mwanza, ikiwa ni miaka minane imepita tangu ATCL ilipositisha safari za ndege zake za Musoma kupisha upanuzi na uboreshaji wa uwanja huo.

Abiria wakipanda kwenye ndege hiyo kabla ya kuruka kutoka Musoma kwenda Dar es Salaam kupitia Mwanza.

Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, ni rasmi sasa ndege za shirika hilo, Air Tanzania, zitakuwa zinatua Musoma mara mbili kwa wiki, yaani Alhamisi na Jumamosi.

Mgeni rasmi katika hafla ya kushuhudia kutua kwa ndege hiyo alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Evans Mtambi, aliyewakilishwa na Katibu Tawala wa mkoa huo, Gerald Kusaya.

"Wakazi wa mkoa wa Mara tumepokea ndege yetu, ni jambo zuri sana, inakuja kuukomboa mkoa wetu si tu katika masuala ya usafiri, lakini katika masuala mazima ya uchumi,” alisema Kusaya na kuendelea:

"Kipekee tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu amekuwa kinara katika kuanzisha safari hizi, kutujengea uwanja na upanuzi mkubwa, kuwalipa fidia wananchi waliokuwa wanakaa maeneo hayo na kuruhusu ndege ya ATCL iweze kufanya safari za huku.”

Katibu Tawala wa Mkoa, Gerald Kusaya (aliyevaa koti na shati la pinki), wafanyakazi wa ATCL na viongozi mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja wakati Air Tanzania ilipotua kwenye Uwanja wa Ndege Musoma jana. (Picha zote na Gazeti la Sauti ya Mara)

Naye Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Mgore Miraji, akizungumza wakati wa tukio hilo la kihistoria, aliipongeza serikali akisema hatua hiyo itafungua fursa za kiuchumi katika mkoa wa Mara.

"Niipongeze serikali ya Tanzania, ndoto imekuwa kweli, leo ni siku ya kipekee sana na adhimu ambayo wengi hawakuitarajia, ni miaka minane ndege ya abiria haijawahi kutua hapa, zimekuwa zikija ndogo ndogo, lakini leo imekuja ndege ya ATCL.

"Wananchi wa Musoma, mkoa wa Mara wataweza kusafiri 'direct' kutoka Musoma kwenda Dar, itapunguza muda, gharama na itafungua fursa za kiuchumi katika jimbo la Musoma mjini,” alisema Mbunge Mgore.

Aliongeza: "Natoa shukrani zangu kwa Serikali ya Awamu ya Sita, Wizara ya Uchukuzi, tabasamu la Rais Samia Suluhu Hassan tumeanza kuliona kwani tutakuwa tukisafiri kutoka Musoma kwenda Dar, na kutoka Dar kuja Musoma kila siku ya Alhamisi na Jumamosi.”

Kwa upande wake Msimamizi simamizi wa Uwanja wa Ndege Musoma, Frank Msofe, alisema: "Tuna furaha kupokea ndege ya Air Tanzania, kama mamlaka tumejipanga vizuri, tunaipongeza serikali kwa kuboresha miundombinu ya kuruka na kutua kwa ndege pamoja na maendeleo yanayoendelea.”

Msofe aliendelea: "Tuko tayari kuhakikisha ulinzi na usalama kwa abiria, ndege na watumiaji wote wa kiwanja, abiria kusafiri na kushuka hapa salama.”

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages