NEWS

Thursday, 17 September 2026

Mwitikio mkubwa uthamini kupisha ujenzi wa TSF mpya Barick North Mara



Mkurugenzi wa Shirika la Sheria na Haki za Binadamu la Tuwakombowe Paralegal, Bonny Matto (aliyevaa kofia ya kaki), akizungumza na wananchi katika eneo la uthamini ili kupisha ujenzi wa TSF Mgodi wa Dhahabu wa North Mara. Kulia aliyevaa kofia nyeusi ni Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Gowele.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
--------------

Kazi ya uthamini wa mali za watu watakaopisha ujenzi wa bwawa la majitaka (Tailings Storage Facility- TSF) mpya katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara linaendelea vizuri, huku mwitikio mkubwa wa watu wanofanyiwa uthamini huo ukishuhudiwa.

Tayari watu zaidi ya 350 wamefanyiwa uthamini wa mali zao ili waweze kulipwa fidia kupisha eneo linalohitajika kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo.

“Mwitikio ni mkubwa na unaridhisha, hadi leo [Septemba 15, 2026] watu 350 wafamefanyiwa uthamini,” Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, aliwambia waandishi wa habari Jumatano iliyopita.

Uthamini huo unafanyika katika vijiji vya Matongo na Nyangoto vilivyopo kata ya Matongo wilayani Tarime, ili kuwezesha mgodi huo kutwaa eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo wa TSF.

Muonekano wa sehemu ya eneo linalofanyiwa uthamini kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa TSF.

Kazi ya uthamini huo ilianza Agosti 24, 2026 na inatarajiwa kukamilika ndani ya siku 60, ambapo eneo lenye ukubwa wa ekari 419 linahitajika ili kujenga mradi huo.

Shughuli hiyo ya uthamini inatekelezwa na wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Kabla ya kuanza uthamini huo, serikali ilishirikiana na mgodi wa North Mara kuendesha mikutano ya kuelewesha na kuhamasisha wananchi wa maeneo hayo kuhusu ujio wa mradi huo.

“Uzuri ni kwamba kazi hii ya uthamini imekuwa shirikishi kuanzia ngazi ya vijiji, kata hadi wilaya,” alisema Meja Gowele.

Moja ya mikutano ya kuelimisha na kuhamasisha wakazi wa vijiji vya Matongo na Nyangoto kuhusu mradi wa ujenzi wa TSF katika mgodi wa North Mara.

Mgodi wa North Mara unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Aidha, katika kuhakikisha haki, uwazi, usawa, sheria na uwajibikaji vinazingatiwa kwa pande zote zinazohusika, Barrick imewashirikisha watetezi wa haki za binadamu kutoka mashirika ya ndani kama waangalizi wa uthamini huo.

“Uwazi ni mkubwa na hata kuna watu wa haki za binadamu na vyombo vingine vya serikali, ikiwemo TAKUKURU ili kuhakikisha haki inatendeka,” alisistiza Meja Gowele.

Wakati uthamini huo unaanza Agosti 24, 2026, Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele, alitangaza katazo la serikali kwa wananchi kutofanya uendelezaji wowote katika eneo hilo ambalo lipo katika leseni ya mgodi huo.

Aidha, aliwataka wataalamu na wasimamizi wa mradi huo kutenda haki na kuhakikisha hakuna udanganyifu wowote unaofanyika hadi hatua ya malipo ya fidia.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akizungumza na wakazi wa vijiji vya Matongo na Nyangoto kuhusu mradi huo wa TSF.

Mradi wa ujenzi wa TSF ni muhimu katika upanuzi na uendelevu wa shughuli za mgodi huo kwa manufaa ya kijamii na kiuchumi.

Kwa mujibu wa Barrick, utafiti wa kitaalamu unaonesha kwamba maisha ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara yameongezeka kutoka mwaka 2030 hadi 2041.

Hivyo, ujenzi wa mradi huo wa TSF unalenga kuendana na uendelevu wa mgodi huo baada ya tafiti za Barrick kurefusha maisha yake.

Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Francis Uhadi, akizungumza katika mkutano wa kuelimisha wakazi wa Matongo na Nyangoto kuhusu mradi wa ujenzi wa TSF.

Kampuni ya Barrick imeendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wanaozunguka migodi yake na taifa kwa ujumla, huku ikiongoza kwa ulipaji wa gawio kubwa serikalini.

Tangu ubia wa Barrick na Twiga uanze mwaka 2019, Barrick imewekeza dola za Kimarekani bilioni 4.79 katika uchumi wa Tanzania, kwa mujibu wa takwimu zilizopo.

Kampuni ya Barrick pia imekuwa ikitekeleza Sera ya Maudhui ya Ndani (Local Content) kwa vitendo, ambapo inafanya ununuzi wa bidhaa za uzalishaji kwa asilimia zaidi ya 90 kutoka kwa wazabuni wa ndani, huku asilimia 96 ya wafanyakazi wake wakiwa Watanzania, wakiwemo wanaotoka maeneo ilipo migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages