
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini, Mwita Seri (katikati aliyeshikilia mche wa mti), Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko (kushoto aliyevaa kofia), Meneja Mahusiano wa mgodi huo, Francis Uhadi (kulia mbele) na wengine katika moja ya matukio ya kupanda miti ya asili kandokando ya Mto Tighite.
Tarime
--------------
Ushirikiano wa Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini na kampuni ya Barrick kupitia mgodi wake wa dhahabu wa North Mara, umefanikisha upandaji wa miti ya asili 47,200 kati ya 50,000 iliyotarajiwa kandokando ya Mto Tighite.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Mwita Seri, mradi huo unalenga kurejesha uoto wa asili na kuimarisha uhifadhi wa mto huo uliopo Nyamongo, wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
“Miti hiyo imepandwa katika eneo lenye ukubwa wa takriban ekari 40,” Seri amewambia waandishi wa habari wilayani Tarime leo.
Amebainisha kuwa eneo lililopandwa miti hiyo ni sehemu ya ekari 100 za kingo za Mto Tighite zinazotakiwa kurejeshewa uoto wa asili kutokana na uharibifu wa mazingira.
Hivyo, upandaji wa miti 47,200 kwenye ekari 40 ni hatua ya awali katika safari ndefu ya kurejesha uoto wa asili wa Mto Tighite uliopo jirani na mgodi wa North Mara.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa North Mara, Apolinary Lyambiko, akipanda mti wa asili kandokando ya Mto Tighite.
Seri amesema mradi huo unatarajiwa kuchangia katika kulinda kingo za mto huo kwa kuzuia mmomonyoko wa udongo na kurejesha mazingira ya asili yaliyoharibiwa.
Mwenyekiti huyo wa Jumuia ya Watumia Maji, ametumia nafasi hiyo pia kuishukuru Barrick North Mara kwa kutoa shilingi milioni 36.7 kuwezesha uanzishaji na utekelezaji wa awali wa mradi huo.
“Barrick wamesaidia sana kufanikisha mradi huu, kwani fedha hizo ziligharimia uoteshaji wa miche ya miti ya asili, upandaji, ulinzi wa awali wa miti hiyo na uwekeji wa nguzo za chuma za uzio wa mradi huo,” amesema Seri.
Aidha, Seri ametoa wito kwa jamii zinazozunguka mto huo kuunga mkono mradi huo kwa kuhakikisha kuwa unafanikiwa bila kuhujumiwa kwa namna yoyote ile.
“Jamii inayozunguka Mto Tighite nayo ina wajibu wa kuonesha ushirikiano na juhudi za kulinda miti iliyopandwa ili iweze kukua na kutimiza lengo la kurejesha uoto wa asili wa mto wetu,” amesema.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwezesha mradi huo kifedha na kitaalamu ili kuhakikisha mafanikio yaliyoanza kuonekana yanaendelea kudumu na kuleta matokeo chanya ya muda mrefu kwa mazingira na jamii.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini, Mwita Seri (kulia aliyevaa shati la drafti), akiongoza shughuli ya upandaji wa miti ya asili kandokando ya Mto Tighite.
Mradi wa kurejesha uoto wa asili wa Mto Tighite unatajwa kuwa na umuhimu mkubwa wa kimazingira kutokana na nafasi ya chanzo hicho cha maji katika mfumo wa ikolojia ya eneo hilo.
Ulizinduliwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka jana kwa lengo la kurejesha uoto wa asili wa mto huo unaotegemewa na maelfu ya watu kwa ajili ya maji ya matumizi ya nyumbani, kunywesha mifugo na shughuli za kilimo.
Juni 5, mwaka huu, Mgodi wa North Mara uliungana na Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini na wakazi wa kijiji cha Matongo kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, kwa kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo.
Wadau hao, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Matongo, Charles Ryoba, walieleza kuridhishwa na ukuaji wa miti iliyopandwa na hatua zinazochukuliwa kurejesha uoto wa asili wa mto huo baada ya kuathiriwa na ukataji wa miti ovyo.
Walisema ushirikiano wa Barrick North Mara na jumuiya hiyo unaweka msingi wa hatua zaidi za kuhusisha jamii, taasisi na wadau wengine katika kukamilisha upandaji wa miti ya asili kwenye ekari 100 za kingo za Mto Tighite.
Mto Tighite ni miongoni mwa vyanzo muhimu vinavyochangia maji katika Mto Mara ambao unamwaga maji yake katika ziwa la kimataifa - Ziwa Victoria upande wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment