
Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mary Daniel Surati, akifurahia jambo katika kikao na wenyeviti wa vijiji na vitongoji, Septemba 11, 2026.
Serengeti
---------------
Mbunge wa Jimbo la Serengeti mkoani Mara, Mary Daniel Surati, ameanzisha utaratibu wa kukutana na viongozi wa ngazi mbalimbali ndani ya jimbo hilo kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi na kuweka mikakati ya kuzitatua.
Septemba 11, 2026, ambapo mbunge huyo kijana alikutana na wenyeviti wa vijiji 78 pamoja na wenyeviti wa vitongoji 24 wilayani Serengeti.

Kikao hicho kilijadili hali ya maendeleo ya jimbo hilo, changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali na namna wanavyoweza kushirikiana katika kuzitafutia ufumbuzi.
Viongozi hao walimpongeza Mbunge Mary kwa kuanzisha utaratibu wa kukutana nao moja kwa moja, wakisema hatua hiyo inaweka mazingira mazuri ya kusikiliza kero za wananchi, kuzifuatilia na kuzipatia ufumbuzi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wenyeviti wa Vijiji Wilaya ya Serengeti, Joseph Mseti, alimpongeza mbunge huyo akisema utaratibu huo utaleta tija na kuongeza ufanisi katika kushughulikia masuala yanayohusu maendeleo na ustawi wa wananchi wa Serengeti.
Aidha, kupitia kikao hicho, wenyeviti hao walipewa taarifa kuhusu mashindano ya Mary Serengeti Cup 2026, ambayo yanalenga kuwapa vijana nafasi ya kushiriki katika michezo, kuibua na kukuza vipaji vyao.
Katika hatua hiyo, viongozi hao waliombwa kuwa walezi wa ligi hiyo katika maeneo yao ili kuhakikisha inafanyika kwa mafanikio na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mbunge Mary aliwashukuru viongozi hao kwa ushirikiano wanaoendelea kumpa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuwatumikia wananchi wa jimbo la Serengeti.

No comments:
Post a Comment