
Makundi ya nyumbu yakivuka Mto Mara
Maadhimisho ya 15 ya Siku ya Mto Mara yanafanyika kuanzia Septemba 12 hadi 15, mwaka huu katika Kaunti ya Bomet nchini Kenya, Wizara inayoshughulikia Jumuiya ya Afrika nchini humo imesema.
Mwaka jana, maadhimisho ya namna hiyo ya kupokezana kila mwaka tangu yaanzishwe mwaka 2012, yalifanyika wilayani Butiama, mkoani Mara, Tanzania.
Uthibitisho wa kufanyika kwa maadhimisho hayo mwaka huu umo kwenye barua ya Julai 16, 2026 iliyotumwa kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Bonde la Ziwa Victoria, Dkt. Masinde Bwire.
Siku ya Mto Mara huadhimishwa ili kufanya tathmini ya pamoja kati ya wataalamu wa uhifadhi wa Tanzania na Kenya kuhusu hali halisi ya ikolojia ya bonde la mto huo kwa maisha endelevu ya watu, wanyama na mimea.
Mto Mara ambao unaanzia nchini Kenya ni chanzo kikuu cha maisha kwa viumbe hai kila mahali unapopita kufikia Ziwa Vicctoria
Maadhimisho ya Siku ya Mto Mara yalibuniwa na Sekretarieti ya Mawaziri wa Bonde la Ziwa Victoria katika kikao chake kilichofanyika Kigali, Rwanda mwaka 2012.
Tanzania na Kenya zimekuwa zikiadhimisha kilele cha Siku ya Mara Septemba 15 kila mwaka kwa kupokezana, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza juhudi za pamoja za uhifadhi endelevu wa Bonde la Mto Mara unaotiririsha maji katika Ziwa Victoria upande wa Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afrika Mashariki ya Kenya, kaulimbiu ya maadhimisho ya 15 yanayofanyika katika Kaunti ya Bomet, inasema "Maisha Mbalimbali, Mto Mmoja: Linda Uhai wa Mto Mara".
Bonde la Mto Mara ni kitovu cha shughuli kama vile kilimo, utalii na uvuvi kwa mamilioni ya wanachi wa Tanzania na Kenya wanaoishi kandokando yake.
Ukiwa na eneo la kilomita za mraba 13,325 na utefu wa kilomita 400, Mto Mara unaanzia misitu ya Mlima Mau nchni Kenya na kumwaga maji yake Ziwa Victoria na kuwa chemichemi ya uhai wa Watanzania.
No comments:
Post a Comment