
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa, Fadhili Maganya, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), mjini Musoma jana Septemba 18, 2026.
Musoma
--------------
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Fadhili Maganya, amekosoa baadhi ya kauli na misimamo inayotolewa na wanasiasa na wanaharakati kuhusu mchakato wa Katiba mpya ya Tanzania, akisema inaweza kuchelewesha mabadiliko yanayotarajiwa.
Maganya aliyasema hayo mjini Musoma jana Septemba 18, 2026 katika mkutano na waandishi wa habari, akieleza kuwa ameamua kutoa maoni yake baada ya kupigiwa simu mara kadhaa na wanahabari wakitaka msimamo wake kuhusu mijadala inayoendelea kuhusu Katiba ya mpya.
Huku akijitambulisha kama mwananchi, Mtanzania na kiongozi mwandamizi wa CCM, Maganya alisema mijadala hiyo imeibuka katika majukwaa tofauti, yakiwamo ya kisiasa, ambapo hoja mbalimbali zikitolewa kuhusu uanzishaji wa mchakato wa Katiba mpya.
Kwa mujibu wa Maganya, baadhi ya washiriki wa mijadala hiyo wametaka mchakato wa mabadiliko ya Katiba uanze haraka na wengine wakisisitiza kuwa mchakato huo ni wa wananchi na haupaswi kugeuzwa kuwa ajenda ya wanasiasa na wanaharakati.
Alisema japo hakushiriki katika majukwaa hayo, lakini amekuwa akifuatilia mijadala hiyo na anaona kuna umuhimu wa Watanzania kutafakari kwa kina namna ya kufikia mabadiliko wanayoyataka bila kuibua mazingira yanayoweza kuuchelewesha mchakato huo.
Akizungumzia msimamo wa baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani, Maganya alisema vimekuwa vikiweka masharti licha ya serikali kuelekeza kuwa maridhiano yatangulie kabla ya kuingia kwenye mchakato wa Katiba.
Alisema kwa mtazamo wake, maridhiano hayapaswi kuhusishwa na chama cha siasa na wanaharakati kwa kuwa yanahusu jamii nzima ya Watanzania.
“Maridhiano siyo ya wanasiasa na wanaharakati, bali ni ya jamii yote ya Watanzania,” alisema Maganya.
Hivyo, kiongozi huyo wa chama tawala - CCM, aliwataka Watanzania kufanya kile alichokiita “home work” kwa kujiuliza iwapo mchakato wa Katiba mpya lazima uhusishe mchakato mrefu na wenye gharama kubwa.
Alisema Watanzania wanapaswa kuangalia iwapo kuna njia nyingine ya kufikia maudhui wanayoyataka kupitia mabadiliko ya Katiba, akisisitiza kuwa hoja muhimu siyo tu namna Katiba inavyotengenezwa, bali pia maudhui yanayoingizwa ndani yake.
Aidha, Maganya alikosoa kauli aliyodai kuwa aliisikia kutoka kwa kada wa chama cha upinzani, kwamba Katiba mpya itaenda “kuijenga nchi upya”.
Kwa mtazamo wake, Maganya alisema kauli hiyo inaweza kutoa picha kwamba Tanzania haipo au haijajengwa, jambo alilolipinga akisisitiza kuwa taifa hilo lipo kwa miaka zaidi ya 60 sasa.
Maganya alihitimisha kwa kusisitiza kuwa hoja ya Katiba mpya ipo, lakini mchakato huo, kwa maoni yake, unapaswa kuzingatia misingi inayolinda utulivu na usalama wa taifa.
“Yes, tunataka Katiba lakini tujikite kwenye misingi ambayo inaweza ikatubakizia taifa letu katika hali salama,” alisisitiza Maganya.
No comments:
Post a Comment