NEWS

Friday, 11 September 2026

Mara wampongeza Mkuu wa Mkoa Brigedia Jenerali Mtambi kwa kupandishwa cheo



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi (katikati) akifurahia picha ya pamoja na viongozi, watumishi wa umma na wadau mbalimbali wakati wa hafla ya kumpongeza kwa kupandishwa cheo, iliyofanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, mjini Musoma, leo Ijumaa, Septemba 11, 2026.

Na Mwandishi Wetu
Musoma
---------------

Viongozi wa serikali, dini, watumishi wa umma na wadau mbalimbali mkoani Mara wameshiriki hafla maalum ya kumpongeza Mkuu wa Mkoa huo, Evans Alfred Mtambi, kwa kupandishwa cheo kutoka Kanali kuwa Brigedia Jenerali wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Hafla hiyo ambayo imeongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Mara, Gerald Kusaya, imefanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, mjini Musoma, leo Ijumaa, Septemba 11, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alimpandisha Mkuu wa Mkoa huyo kuwa Brigedia Jenerali, cheo ambacho alianza kukitumikia kuanzia Agosti 21, 2026.

Akizungumza katika hafla hiyo ya kumpongeza Brigedia Jenerali Mtambi, DAS Kusaya ametoa shukrani za dhati kwa Rais Samia kwa kuendelea kuupa kipaumbele mkoa wa Mara na kuwaamini viongozi wenye uwezo na uadilifu.

Amesema kupandishwa cheo kwa Mkuu wa Mkoa huyo ni ishara ya kutambua weledi, uhodari, utii na utumishi wake uliotukuka katika kulitumikia taifa.

“Tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa kuendelea kuupa kipaumbele mkoa wa Mara. Kupandishwa cheo kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa ni heshima kubwa kwetu wana-Mara na ni uthibitisho wa kutambua weledi, uadilifu na ushupavu wake katika kulitumikia taifa,” amesema Kusaya.

Naye Mkuu wa Mkoa, Brigedia Jenerali Mtambi amemshukuru Rais Samia kwa kumwamini na kumpa nafasi ya juu ya uongozi wa jeshi.

Pia, amewashukuru viongozi wenzake wa serikali, dini watumishi wa umma na wananchi wote wa mkoani Mara kwa maombi yao, ushirikiano na kuendelea kumuunga mkono katika kutekeleza majukumu yake.

“Ninamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuniamini na kunipa nafasi hii. Nawashukuru pia viongozi wenzangu, viongozi wa dini, watumishi wa umma na wananchi wote wa Mara kwa maombi, ushirikiano na kujitoa kwao katika kulitumikia taifa,” amesema Brigedia Jenerali Mtambi.

Katika hafla hiyo, DAS Kusaya amemkabidhi Brigedia Jenerali Mtambi ngao ya pongezi kwa niaba ya wana-Mara. Aidha, hafla hiyo pia imeambatana na tukio la kukata keki, ikiwa ni sehemu ya kuonesha furaha na pongezi kwa Mkuu wa Mkoa huyo.

Mkuu wa Mkoa Brigedia Jenerali Mtambi akikata keki katika hafla hiyo ya kumpongeza kwa kupandishwa cheo. (Na Mpigapicha Wetu)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages