NEWS

Sunday, 6 September 2026

Meneja wa Barrick Tanzania aishukuru jamii inayozunguka Mgodi wa North Mara kwa mahusiano mazuri



Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa helikopta ya utafiti wa madini na Programu MBT, uliofanyika Nyamongo wilayani Tarime, Agosti 31, 2026. (Na Mpigapicha Wetu)

Na Mwandishi Wetu
Tarime
------------

Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, amewashukuru wakazi wa vijiji vilivyo jirani na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa mahusiano mazuri baina ya pande hizo mbili.

“Tunaishukuru jamii ya hapa North Mara kwa kuwa jirani na sisi,” alisema Dkt. Ngido katika hafla ya uzinduzi wa utafiti wa madini kwa kutumia helikopta ya kampuni ya Barrick.

Uzinduzi huo ulifanyika sambamba na unzinduzi wa Programu ya Madini kwa Kesho Njema (Mining for a Brighter Tomorrow - MBT) katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime, Agosti 31, 2026.

Kiongozi huyo wa Barrick Tanzania alionesha kufurahishwa na wananchi wanaoishi jirani na mgodi huo kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakishirikiana nao katika miaka ya hivi karibuni.

Aliwashukuru pia viongozi wa vijiji na kata kwa ushirikiano wao kwa Mgodi wa Barrick North Mara na hivyo kuufanya uwekezaji huo kuendelea kuwa na tija katika kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika vijiji hivyo na taifa kwa ujumla.

“North Mara imebadilika sana, tunajisikia furaha, na tunaomba jamii kuendelea kutupatia ‘support’ ili kuleta manufaa zaidi,” alisema Dkt Ngido.

North Mara ni moja ya migodi mikubwa ya dhahabu inayoendeshwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa Mgodi wa North Mara umetumia shilingi bilioni 26.86 kugharimia utekelezaji wa miradi 255 katika sekta za elimu, afya, barabara, maji, kiuchumi na mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime tangu mwaka 2019 ulipokabidhiwa kwa Barrick.

Miradi hiyo imetekelezwa chini ya mpango wa Barrick wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Mgodi mwingine unaoendeshwa na kampuni hiyo ya kimataifa chini ya ubia huo ambao unatajwa kuwa wa mfano wa kuigwa ni Bulyanhulu uliopo katika wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga.

Mbali na kutumia mabilioni ya fedha kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kupitia mpango wa CSR, migodi hiyo inaelezwa kuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa kwa kulipa kodi na kutoa gawio serikalini.

"North Mara na Bulyanhulu ndio walipaji wakubwa wa kodi nchini, na ndio migodi inayoongoza kwa kutoa gawio kubwa serikalini.

“Tutaendelea kushirikiana na serikali, Wizara ya Madini na jamii inayotuzunguka. Tunaleta maendeleo, tunatoa ajira na kukuza uchumi wa jamii," alisema Meneja Mkazi huyo wa Barrick hapa Tanzania.

Tangu ubia wa Barrick na Twiga uanze mwaka 2019, Barrick imewekeza dola za kimarekani bilioni 4.79 katika uchumi wa Tanzania kupitia kulipa kodi na tozo mbalimbali, gawio, mrabaha, mishahara, malipo ya wazabuni wa ndani na utekelezaji wa miradi ya kijamii, kwa mujibu wa takwimu zilizopo.

Barrick pia imekuwa ikitekeleza Sera ya Maudhui ya Ndani (Local Content) kwa vitendo, ambapo inafanya ununuzi wa bidhaa za uzalishaji kwa asilimia zaidi ya 90 kutoka kwa wazabuni wa ndani, huku asilimia 96 ya wafanyakazi wake wakiwa Watanzania, wakiwemo wanaotoka maeneo ilipo migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu.

Aidha, viongozi wote wa nafasi za juu katika uendeshaji wa shughuli zake hapa nchini kwa sasa ni Watanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages