
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, akizungumza na waandishi wa habari.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema jitihada za kudhibiti moto uliozuka katika Mlima Kilimanjaro zimefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 90, huku hatua zaidi zikiendelea kuchukuliwa kuhakikisha moto huo unadhibitiwa kikamilifu na kuepusha madhara zaidi.
Dkt. Kijaji ametoa taarifa hiyo leo Jumamosi, Septemba 5, 2026, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya shughuli za udhibiti wa moto huo na kujiridhisha na hatua iliyofikiwa.
Amepongeza vikosi vya Jeshi la Uhifadhi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali kwa juhudi kubwa wanazofanya kufanikisha udhibiti wa moto huo.

Aidha, Waziri Kijaji amewataka waongoza watalii na watalii kuchukua tahadhari na kushiriki katika kulinda mazingira kwenye hifadhi zote nchini.
Amewataka pia wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopakana na hifadhi zote nchini kujiepusha na shughuli zinazoweza kusababisha au kuchochea moto ndani ya hifadhi.
Amebainisha kuwa shughuli za utalii katika Hifadhi ya Taifa Mlima Kilimanjaro zinaendelea kama kawaida, huku serikali ikiendelea kuchukua hatua kuhakikisha usalama wa watalii na waongoza watalii wakati wote.
Katika ziara hiyo, Waziri Kijaji amefuatana na Kamishna wa Uhifadhi wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Mwishawa, ambaye amemhakikishia kuwa hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kuhakikisha moto huo unadhibitiwa kikamilifu.

Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Mwishawa.
No comments:
Post a Comment