
Hafidh Ameir Hassan enzi za uhai
Na Mwandishi Wetu
Hafidh Ameir Hassan, mume wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefariki dunia mapema leo Jumatatu, Septemba 7, 2026.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, imeeleza kuwa Hafidh ameaga dunia akiwa anapatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena, Zanzibar.
Akitoa salamu za pole, Makamu wa Rais alisema: "Ninatoa pole kwa Mheshimiwa Rais, familia, ndugu, jamaa na marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu, na mpango wa mazishi unaendelea kufanyika Kizimkazi."
Kwa miaka mingi, Hafidh aliishi maisha ya faragha, akiwa mbali na siasa na vyombo vya habari. Hata pale aliposhiriki katika baadhi ya shughuli pamoja na mke wake, hakujitokeza sana.
Mchambuzi kutoka Zanzibar, Rehema Mema, anamwelezea Hafidh kama mtu mpole, mkarimu na asiye na tamaa ya kujulikana.
"Ni baba ambaye hapendi kujulikana, mwenye mambo mengi, mpole, mkarimu, asiyependa makuu. Kama angekuwa baba mwingine, tungekuwa tunamfahamu sana."
Hafidh alikuwa mtaalamu wa masuala ya kilimo na mstaafu wa taaluma hiyo. Alifunga ndoa na Samia Suluhu Hassan mwaka 1978 na walipata watoto wanne.
Miongoni mwa watoto wao ni Wanu Hafidh Ameir, mwanasiasa ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Jimbo la Makunduchi na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mipango ya mazishi ya Hafidh Ameir inaendelea kufanyika Kizimkazi, Zanzibar.
No comments:
Post a Comment