NEWS

Saturday, 12 September 2026

Ushirikiano wa Tanzania, Algeria wazidi kuzaa matunda, wanafunzi 150 kupata ufadhili



Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mobhare Matinyi.

Na Mwandishi Wetu

Mkazo mkubwa unaowekwa na serikali kwenye masomo ya sayansi, sasa umeanza kupata msukumo zaidi kufuatia vijana wa Kitanzania 150 waliofanya vizuri katika nyanja hiyo kupata ufadhili wa Serikali ya Algeria.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojiia, Prof. Adolf Mkenda, amewaambia waandishi wa habari juzi kuwa Serikali ya Algeria itatoa ada za masomo wakati Serikali ya Tanzania itatoa fedha za kujikimu chini ya mpamgo wa Samia Scholarship.

Samia Scholarship ni mpango maalum wa ufadhili kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita kwa masomo ya sayansi.

Huu ni mpango wa kuwezesha vijana kutoka familia duni ili taifa lijipatie wataalamu wa kutosha katika fani ya sayansi.

Kwa mujibu wa Prof. Mkenda, mpango huo wa Samia Scholarship unajumuisha wanafunzi 10 waliochaguliwa kwenda Urusi.

Mwaka jana, wanafunzi 45 walikwenda kusoma Algeria kabla ya ongezeko la sasa kufikia wanafunzi 150.

Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mobhare Matinyi, ameishukuru nchi hiyo kwa kuongeza nafasi za masomo kwa Watanzania na kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

Balozi Matinyi amesema Watanzania waliochaguliwa utabidi wajifunze lugha ya Kifaransa, lugha ambayo ni muhimu kwa mawasiliano na mafunzo katika fani mbalimbali.

Ameeleza kuwa Ubalozi wa Tanzania utashirikiana na wizara husika kuhakikisha kuwa wanafunzi waliochaguliwa wanatimiza azima ya taifa ya kuwa na wataalamu wengi wa sayansi na TEHAMA.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages